Na Mwandishi Wetu, Mbarali


BAADHI ya wazee wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wamelalamikia vitendo vya vijana  wao, kuzalia nyumbani na kuwatelekezea watoto hali inayowapa mzigo wa kuwalea.


Wameyasema hayo juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee ambayo katika wilaya hiyo yalifanyika katika kata ya Mahongole yakiwa na kauli mbiu ya ‘tupaze sauti kupinga ukatili kwa wazee’.


Akisoma risala kwa niaba ya wenzake katibu wa baraza la wazee wilayani Mbarali, Michael Sanga alisema kuwa vijana wao wamekuwa na tabia ya kuwatelekezea watoto wao nyumbani na wao kwenda sehemu nyingine kutafuta maisha hali ambayo inawaongezea ugumu wa maisha.


“Kuna tabia sio nzuri ya vijana wetu kutuachia wajukuu na wao kuondoka, ukizingatia maisha yetu wazee ni magumu, kama wao tuliwalea kwa nini wato watutelekezee watoto wao nyumbani kwetu hii sio sawa kabisa”, alihoji.


Katika hatua nyingine Sanga aliiomba serikali kuweka sheria itakayoziwezesha halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha wazee ili waweze kujikwamua kiuchumi kama inavyofanya kwenye makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.


Sanga alisema kumekuwa na dhana kuwa wazee hawana sifa ya kukopesheka kutokana na umri wao na kwamba mtazamo huo ni ukatili dhidi ya kundi hilo ambalo linapaswa kuwezeshwa kiuchumi.


“Tunanyimwa mkopo na halmashauri eti hatukopesheki huo ni ukatili kwa wazee, tumeona vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanatengewa asilimia na hamashauri isipokuwa sisi hii haijakaa sawa,’’ alisema


Kwa upande wake mwenyekiti wa barala za wazee katika halmashauri hiyo, Hezron Kapwela aliwataka vijana kuacha tabia ya kuuza mashamba yao kwani huo ndio urithi wao kwa sasa na miaka ijayo.


Aliwataja vijana wanaouza mashamba kuwa wamepitwa na wakati na kuwataka kuiga mfano wa wazee wao kwani  nao wangeyauza enzi za ujana wao watoto wao wasingeyakuta.


Mkuu wa wilaya ya Mbarali Reuben Mfune alisema kitendo cha vijana kuwatelekeza watoto wao kwa wazazi kunachangia wimbi la umasikini na kuwasihi kujipanga vyema kabla ya kuzaa ili waweze kuwatunza badala ya kuwapa mzigo wazee.


Mfune ambaye aliwakilishwa na mkuu wa idara ya mazingira katika halmashauri hiyo, Raphael Shitindi alisema pamoja na mambo mengine ataziwasilisha changamoto za wazee hao ngazi za juu kwa ajili ya kushughulia.


SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya wazee wilayani Mbarali (KIWWAUTA)limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia wazee wilayani humo  pamoja na kusimamia masuala mbali mbali ya wazee.


Mwisho.

Share To:

Post A Comment: