Rais Samia  Suluhu Hassan.
Mjumbe wa Wachimbaji Madini Dodoma , Said Shabani


Na Dotto Mwaibale, Dodoma


WACHIMBAJI wadogo wa madini kutoka Kijiji cha Yobo, kitongoji cha Yobo Kata ya Anet iliyopo Chamwino Dodoma wamlilia Rais Samia Suluhu Hassan awapatie eneo la kuchimba madini ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuiingizia serikali mapato. 

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Hussein  Kimolo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wananchi 300 waliounda umoja wa vikundi 14 vya wachimbaji.

Kimolo alisema wameamua kupeleka ombi lao kwa rais baada ya kulifikisha kwa watendaji wengine wa serikali bila mafanikio.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, tayari wameanza kuchimba madini kwenye eneo lisilo na tija walilopewa na wizara ya madini, baada ya kuona hawanufaiki kiuchumi zaidi ya pesa wanazopata kuishia kulipa mapato ya serikali walipeleka ombi lao kwa viongozi kadhaa il wapewe viwanja vitatu vyenye tija bila mafanikio.

Akielezea kwa undani sababu iliyowafanya wamililie Mama Samia awepe eneo la kuchimba madini, Kimolo alisema shughuli hiyo ya uchimbaji wanaifanya baada ya kukata leseni za kuchimba madini aina ya nikeli kwenye viwanja vitano kati ya tisa ambavyo mzungu raia wa Ugiriki aitwaye Milcan Dimist ana vimiliki alivyovikatia leseni nane zenye ukubwa usiopungua hekta 6 kwa kila leseni.

“Tuliomba viwanja hivyo vitano na kukata leseni kufuatia mzungu huyo tangu aliporithi viwanja hivyo kwa baba yake ambaye ni marehemu miaka zaidi ya 33 iliyopita kushindwa kuchimba kwenye viwanja vyote isipokuwa kimoja tu.

Alisema baada ya kubaini jinsi serikali inavyokosa mamilioni ya fedha za kodi kupitia mzungu huyo kushindwa kuchimba kwenye viwanja hivyo walimuomba waziri wa madini atugawie viwanja vitano kutoka anavyomiliki mzungu huyo ambapo alitushauri tuunde vikundi na kukate leseni.

“Tangu tulipokata leseni hizo mwaka 2019 tumepewa viwanja viwili ambavyo ni namba PML 0382 D0M na namba PML 0381 hadi leo hatujapewa vitatu vilivyobaki hivyo kupata hasara ya kulipa mapato ya serikali bila ya kuzalisha chochote kwa upande wetu,” alisema Kimolo.

Kiongozi huyo amesema, licha ya kumwandikia barua ya malalamiko Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli na kuipeleka ofisini kwake jinsi ambavyo viongozi walivyoshindwa kuwasaidia kupata viwanja hivyo hakuna kilichoendelea hadi leo jambo linalowafanya waamini aliyeipokea hakuipeleka mezani kwake kwani kama rais huyo aliyekuwa mtetezi wa wanyonge angeyapata angeingilia kati na wangekuwa wamepewa viwanja hivyo vyenye tija ambapo wangeliingizia taifa letu fedha nyingi.

“Kinachoshangaza ni sisi kushindwa kupewa viwanja hivyo na kuishia kusumbuka kwenda kwa viongozi mara kwa mara kuwalilia wasikie kilio chetu bila mafanikio wakati tunaishi Wilaya ya Chamwino ambayo ina makazi ya rais wetu ambapo tulishuhudia viongozi akiwemo Hayati Magufuli, Waziri Mkuu, Waziri Wililam Lukuvi, Rais Mama Samia wanavyowasaidia wananchi sehemu mbalimbali nchini kupata haki zao zinazohusiana na migogoro ya ardhi na machimbo ya madini,” alisema mwenyekiti huyo.

Aliongeza kuwa, hawana nia mwekezaji huyo aporwe viwanja vyote kwani itakuwa si kumtendea haki kwa sababu serikali inawahitaji wawekezaji isipokuwa wapewe viwanja hivyo vitatu walivyoviomba vikiwemo viwili wanavyochimba visivyo na tija ili mzungu anayemiliki hekta zaidi ya 97 za ardhi yenye madini abaki na vinne licha ya kuwa na uwezo wa kuchimba katika kiwanja kimoja tangu alipoanza kuchimba madini hayo zaidi ya miaka 33 iliyopita.

“Tunamuomba Mama Samia atusaidie tupate viwanja vilivyosalia ili tuiingizie serikali yetu mapato huku na sisi tukiinua vipato vya familia zetu kwani umoja wetu wa watu 300 unawakilisha kundi kubwa la watu,” alisema mwenyekiti huyo. 

“Tunamuomba rais wetu mama Samia anayeelewa changamoto za kiuchumi tunazozipata sisi watu wa chini atusaidie kupata viwanja hivyo au atuite viongozi wa umoja huo tutamueleza mengi yanayohusu mgodi huo kwa maslahi ya taifa letu,” alisema Kimolo.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko alipogiwa simu mara kadhaa ilikuzungumzia suala hilo  hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya simu hakujibu.

Share To:

Post A Comment: