Shirika lisilo la Kiserikali la Agri Thamani Neema Lugangira ambaye pia ni MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) akisisitiza jambo wakati wa semina hiyo








WABUNGE wameishauri Serikali kurudisha mashuleni somo la sayansi kimu ili watoto wafundishwe kuandaa lishe bora tangu wakiwa watoto, jambo ambalo litasaidia kupambana na athari zitokanazo na lishe duni.

Akizungumza katika semina lishe kwa Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG), iliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Agri Thamani, Mbunge wa Urambo (CCM) Magareth Sitta alisema zamani watoto walifundishwa juu ya kutayarisha chakula lakini hivi sasa hawajifunzi tena.

“Serikali kwanini wameondoa somo la domestic sience (sayansi kimu) sisi wengine tulijifunza kule namna ya kuandaa chakula. Na kwanini wanafunzi hawana mashamba ya shule,”alisema.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Anna Lupembe aliunga mkono kauli ya Sitta ambaye alitaka wataalam wa lishe kutembea katika halmashauri kwa ajili ya kutoa elimu ya lishe bora.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema suala la lishe ni muhimu sana halifai kuchukuliwa kiwepesi.

Alitaka suala la lishe na magonjwa ya kuambukizwa kupelekwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ili yaweze kuratibiwa kikamilifu.

Mkurugenzi wa shirika hilo Neema Lugangira alisema udumavu unaotokana na lishe duni unaleta unasababisha uwezo mdogo wa kufyonza virutubishi  na uyeyushaji wa chakula.

Alitaja athari nyingine ni riski ya kupata magonjwa mbalimbali hasa ya kuambukiza, kuugua mara kwa mara kwa mtu mmoja mmoja na kwa familia, gharama kubwa ya matibabu.

“Ongezeko kwa kasi ya ugonjwa mfano Ukimwi kiwemo mama mwenye Ukimwi kumuambukiza mtoto Ukimwi. Elimu duni haswa kwa vijana,”alisema.

Alisema udumavu unaweza kupunguza uwezo wa kufikiri wa mtu na upungufu wa madini joto, unaweza kupunguza, kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu na upungufu wa wekundu wa damu

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Dk Thea Ntara alishauri wataalam wa lishe nchini kufanya utafiti wa vyakula vinavyoweza kumpatia mtu vitamin E.

Mbunge wa Mkinga (CCM) Dustan Kitandula alisema fedha zinazotengwa na halmashauri kwa ajili ya lishe zimekuwa hazitumiki katika shughuli iliyokusudiwa.

Alishauri Serikali kutenga fedha za lishe katika bajeti kuu ya Serikali na kuziwekea uzio badala ya utaratibu wa sasa wakuziachia halmashauri kupanga bajeti hiyo.

Mbunge wa Iringa (CCM) Jesca Msambatavangu aliwataka wataalam wa lishe nchini kufanya utafiti katika mbegu za asili zinazopatikana katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha lishe.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Agri Thamani na Mbunge Neema Lugangira alisisitiza kuwa lengo la Semina ya Lishe Bora kwa Wabunge ni kuhakikisha kwamba Ajenda ya Lishe Bora inakuwa ya kipaumbele, inazungumziwa na inafuatiliwa kuanzia ndani ya Bunge hadi kwenye Mabaraza ya Madiwani ngazi ya Wilaya ambapo Kila Mbunge ni Diwani katika Wilaya yake. 

Hata hivyo alisema kwamba ni  matumaini yake kwamba ndani ya Miaka 5 hii 2020-2025 Tanzania itapata Mageuzi Makubwa Katika Suala zima la Lishe Bora na kupunguza kwa kiasi kubwa Udumavu na aina zote za Utapiamlo nchini

Mwisho

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: