Na Mwandishi wetu-Ushetu



Waziri wa Madini,  Doto Biteko ameagiza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama kwa kushirikiana na Afisa Madini kukutana ili kujadiliana uwezekano wa kuwapatia wananchi walioomba eneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini lililopo katika eneo la shule ya Msingi Mwabomba, Kata ya Idahina katika Halmashauri ya Ushetu.


Waziri Biteko ametoa agizo hilo leo tarehe 7 Mei 2021 wakati akizungumza na wachimbaji wa madini akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga huku akisisitiza katika kikao hicho kiwahusishe viongozi wa serikali ya kijiji.


Amesema kuwa pamoja na kwamba eneo hilo la uchimbaji lipo katika shamba la shule lakini upo uwezekano wa kuihamisha shule hiyo ikajengwa katika ubora zaidi jambo ambalo litaruhusu uchimbaji kuendelea kwani serikali itajipatia mapato.


“Kuna maneno yanazungumzwa kuwa wanachimba kwenye shule, kwanza sio shule ni kwenye shamba la shule, na hilo sio eneo la kwanza yapo maeneo mengi yaligundulika yana dhahabu tukahamisha shule tukachimba madini na shule nzuri ikajengwa” Amekariri Waziri Biteko


Amesema kuwa kuihamisha shule sio jambo la ajabu badala yake amesisitiza ulazima wa kujiridhisha endapo hiyo shule itafidiwa na kujengwa shule nyingine bora kuliko iliyokuwepo.


Waziri Biteko ameungana na wananchi kuonyesha ulazima wa kuwapatia wananchi eneo hilo kwa ajili ya uchimbaji kwani kumekuwa na uchimbaji holela ambao hauna manufaa kwa wananchi.


Amewataka wananchi hao kuwa na subira kwani jambo hilo litafikiwa muafaka hivi karibuni huku akiwataka wananchi hao kuacha tabia ya uchimbaji nyemelezi usiokuwa na ruhusa kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu na sheria za nchi.


Kadhalika, amekemea tabia ya wachimbaji wadogo kuchukiana ambapo amesisitiza wananchi hao kuchimba madini kwa umoja, ushirikiano na upendo.


Kwa upande wake Kamishna wa madini Mhandisi David Mulabwa amewataka wachimabji hao   kuendelea kutii na  kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Sekta ya Madini nchini.


Mhandisi Muhabwa amesema kuwa pamoja na kupata fedha kutokana na shughuli hiyo ya uchimbaji lakini pia wanapaswa kuzingatia masuala ya afya, usalama na uhifadhi wa mazingira.


Naye Kamishna wa Tume ya Madini Prof Abdulkarim Mruma amempongeza aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli kwa kufanikisha na kuwatambua wachimbaji wadogo wa madini sambamba na kuwawezesha wachimbaji kote nchini.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: