Mtambo wa uchimbaji wa visima wa Kampuni ya Ahia General Supplies, ukiwa kwenye eneo la shamba la ekari mbili la mradi wa kilimo cha mbogamboga katika Kata ya Kipumbwiko wilayani Ikungi mkoani hapa. Mradi huo unaendeshwa na  Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.
Mshauri na Msimamizi wa uchimbaji wa visima vya mradi huo ambavyo vinachimbwa na Kampuni ya Ahia General Supplies, Hezron Philip, akizungumzia manufaa ya mradi huo na mchakato mzima wa uchimbaji wa kisima hicho.
Mtaalamu wa Kilimo wa TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari, akiwaelekeza jambo wataalamuwa uchimbaji wa visima wa Kampuni ya Ahia General Supplies. Kushoto ni Mratibu wa Mradi wa UN WOMEN, Glory Prosper.
Wananchi wa Kata ya Kipumbwiko, wakisaidia kuweka matawi ya miti barabarani ili kuwezesha gari lenye mtambo wa uchimbaji wa kisima liweze kupita.
Gari lenye mtambo wa uchimbaji wa kisima likielekea kwenye eneo la mradi.
Mtambo wa uchimbaji wa kisima ukitoa maji.
Muonekano wa shamba la mradi.
Fundi wa mtambo wa uchimbaji wa kisima wa Kampuni ya Ahia General Supplies, akiwa kazini.



Na  Dotto Mwaibale, Singida 



 ASASI kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA imeanza mchakato wa kuchimba kisima cha maji katika Kata ya Kipumbwiko wilayani Ikungi mkoani hapa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kuanza kilimo cha mbogamboga.

 Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa  mshauri na msimamizi wa uchimbaji wa visima vya mradi huo ambavyo vinachimbwa na Kampuni ya Ahia General Supplies, Hezron Philip alisema kisima hicho chenye urefu wa mita 100 kwenda chini kikikamilika kitakuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wananchi wa kata hiyo hasa wanawake.

"Baada ya kukamilika kwa kisima hiki kitakacho wanufaisha wanawake wa vikundi vinne vilivyopo ndani ya mradi  katika  Kijiji cha Kipumbwiko kwa uzalishaji wa mboga mboga kwa njia ya kilimo cha umwagiliaji kitawapa wananchi matumaini ya maisha" alisema Philip.

Alisema maji yatakayopatika katika kisima hicho ni kuanzia lita 5000 kwa saa hivyo kuwa na uhakika wa kuendesha kilimo hicho. 

"Kisima hiki ambacho tutakijenga kwa ubora wa hali ya juu kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuwepo zaidi ya miaka 100 hivyo  wanakikundi watarajie mafanikio makubwa kwani maji yatakuwepo ya kutosha kwa masaa 24." alisema Philip.

Philip alitoa mwito kwa wananchi kutunza chanzo cha maji ambacho ndio maendeleo na kuwa kisima hicho kitakuwa shamba darasa ambapo wananchi watajifunza kuwa na maji wataweza kuwa na maisha bora na maendeleo katika jamii.

 Mradi wa kilimo hicho unaendeshwa na TAHA kwa kushirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa ni kuwakomboa wanawake  kiuchumi.

 TAHA inaendesha kazi zake katika mikoa 25 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja

 ( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba  ( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini )  Ikungi-Singida na  Msalala-Shinyanga.

 Asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi. 

Wadau wanao wezeshwa katika mnyororo huo wa thamani ni wasambazaji wa pembejeo, wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na makampuni yanayofanya usafirishaji nje ya nchi na wanawawezesha kwa vitendo.

Kazi kubwa zinazofanywa na TAHA ni nne kwanza  ni kuwaunganisha wakulima na masoko, kuwawezesha wakulima katika suala zima la kilimo na kuwaonesha teknolojia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kulingana na uwezo na mazingira waliopo. 

Tatu ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kwa maana ya kushawishi na kutetea sera

zile ambazo zinamuumiza mzalishaji, mfanyabiasha na mdau yeyote katika mnyororo wa thamani.

Kazi ya nne na ya mwisho ni kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na vyombo vya fedha baada ya kuwafundisha elimu ya fedha.

Share To:

Post A Comment: