Imeelezwa kuwa, Vitengo vya Mawasiliano Serikalini ndiyo Mdomo wa Wizara au Taasisi na Mkono unaopokea taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya Habari hivyo, vimetakiwa kujiendesha kitaalamu.


Hayo yamesemwa leo Mei 21, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila wakati akifunga Kikao Kazi cha kujadili na kuboresha Mkakati wa Mawasiliano wa Wizara ya Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Abdulkarim Mruma jijini Dodoma.


Prof. Msanjila amesema, Vitengo vya Mawasiliano vina umuhimu mkubwa wa kuzitangaza Wizara na Taasisi zao hivyo kuwataka Maafisa Habari walioshiriki Kikao hicho kushirikiana na kupeana taarifa mbalimbali zinazohusu Sekta zao  ili kuwa na uelewa wa pamoja wa majukumu ya Serikali ikiwemo kupeana mikakati inayolenga kuboresha utoaji taarifa za Serikali.


“Maafisa habari niwaombe muongeze ushirikiano baina yenu na mjitahidi kuwa na taarifa za Wizara ama Taasisi nyingine ili kuongeza wigo wa Mawasiliano.


Ukizungumzia CSR na Local Content TAMISEMI lazima wawe ndani,” amesema Prof. Msanjila.


Aidha, Prof. Msanjila amewataka maafisa hao kutumia kikao hicho kujijengea uwezo na kuongeza uzalendo ili kuongeza tija katika utendaji wao wa kazi ikiwemo kuziuza rasilimali mbalimbali zinazopatikana nchini.  


Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini Asteria Muhozya, amewapongeza Maafisa Habari walioshiriki kikao hicho kutokana na michango iliyotolewa  ambayo inatarajia kuboresha zaidi mkakati huo unaotajwa kuwa dira ya utoaji elimu katika Sekta ya Madini.


Awali, akiwasilisha Mkakati huo, Muhozya amewataka wadau hao kuwa huru katika kutoa maoni  ili kuwezesha  kupatikana  kwa mkakati bora ambao utaleta tija kwenye Sekta ya Madini ikizingatiwa umuhimu wa sekta hiyo katika maendeleo ya nchi ikiwemo kuchagia na kukuza sekta nyingine kiuchumi.


Kikao kazi hicho kimehudhuriwa wa Maafisa Habari na Mawasiliano kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali  za Serikali.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: