Na Mwamvua Mwinyi,Pwani


TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU ),imekagua miradi 15 ya maendeleo katika sekta ikiwemo TASAF ,maji elimu na ujenzi iliyogharimu Bilioni 2.296.583.3 na baadhi ya miradi hiyo imebainika kuwa na dosari.

Aidha taasisi hiyo imeokoa, fedha milioni 134.814.7 ambazo ilikuwa zichepushwe ama kufanyiwa ubadhirifu kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Akitoa taarifa ya robo ya mwaka,kamanda wa TAKUKURU Pwani-Suzan Raymond alisema wameokoa mamilioni hayo ikiwa pia ni pesa za mafao ya watumishi na miradi ya maendeleo.

Alieleza ,kati ya miradi iliyofuatiliwa na kukutwa na kasoro ni pamoja na ujenzi wa chuo cha VETA huko Mafia ambapo maelekezo yalitolewa kwa mamlaka husika ili miradi iweze kuleta matokeo chanya na tija kwenye jamii.

Hata hivyo ,kamanda huyo wa TAKUKURU anafafanua ,fedha zilizotaka kuchepushwa ,kati ya milioni 134.814.7 ,TAKUKURU Bagamoyo iliokoa milioni 57.722.7 michango ya mafao ya NSSF  na PSSSF kwa watumishi wa shule ya sekondari Eagle.

"Fedha hiyo ilichepushwa na haikuwasilishwa na mwajiri ambae ni mmiliki wa shule hiyo ," ofisi ilifuatiliwa na mwajiri alilipa fedha kwa wahusika ili wapate mafao yao.

Pia alisema ,milioni 14 ziliokolewa na kutumika kuchimba visima vinne Bagamoyo ,fedha ambazo zilitolewa kwa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na mfadhili ,Raia wa Oman kwa ajili ya wananchi wa Zinga.

"Tangu fedha zilipotolewa visima havikuchimbwa hivyo tulipata taarifa tulifuatilia na kuhakikisha hazifanyiwi ubadhirifu na kuchimba visima"

Suzan anaongoza ,kuwa licha ya hayo Mkuranga waliweza kuokoa milioni 21.790 ambazo wakulima walidhulumiwa na viongozi wa bodi za AMCOS za Njopeka,Chungulo,Njianne na Tunduni Magawa.

Akizungumzia fedha zilizorejeshwa baada ya kufuatili mikopo iliyotolewa katika vikundi vya wanawake,vijana na walemavu , alitaja halmashauri ya wilaya Kibiti ilitoa fedha 550,000 na vikundi hivyo vilishindwa kurejesha .

Fedha nyingine ni milioni 2.600.0 zilizokopeshwa kwa vikundi katika halmashauri ya wilaya ya Rufiji.

Suzan aliwasihi wananchi kuepuka vitendo vya rushwa kwani dhamira ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu ni kuhakikisha rushwa inatokomea nchini na kwamba ubadhirifu na rushwa ni mwiba unaochoma na kuathiri maendeleo na uchumi wa nchi.

 
Share To:

Post A Comment: