Afisa Mkuu wa Fedha wa TANESCO, Renatha Ndege (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa, Flora Nusu Kitabu ikiwa ni mojawapo ya msaada na zawadi ambazo zimepelekwa na wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO shuleni hapo leo.


Wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhi magodoro, mashuka na chandarua kwa ajili ya Zahanati ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa ikiwa ni kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake duniani Machi 8.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa wakionesha umahiri wao kwenye mchezo wa Sarakasi leo walipotembelewa na wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO na kupatiwa msaada wa mahitaji mbalimbali.
Wanawake kutoka Shirika la Umeme Tanzania TANESCO wakiwa katika picha ya pamoja na Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa walipofika kuwatembelea na kuwapelekea mahitaji mbalimbali kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake duniani.


KATIKA kuadhimisha siku ya Wanawake duniani, Umoja wa Wanawake wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO, wamefanya ziara ya kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa ambapo wametoa misaada ya mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Vifaa na mahitaji yaliyotolewa na Wanawake hao wa TANESCO ni pamoja na Vitabu vya masomo yote, Magodoro, Mashuka, Chandarua, Vifaa vya Michezo , Vifaa vya Usafi na Taulo za Kike ambapo jumla yake yote ni Sh Milioni Sita.

Akizungumza na viongozi na wanafunzi wa shule hiyo, Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Afisa Mkuy Fedha wa TANESCO, Renatha Ndege  amewataka wanafunzi hao kujikita katika kutengeneza ndoto zao kwa kusoma kwa bidii ili kuwa sehemu ya wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali hapo baadaye.

Ndege amesema mafanikio yoyote yanayoonekana nchini na duniani kote kwa kiasi kikubwa pia yamechagizwa na uwepo wa wanawake huku pia akimpongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuendelea kuwaamini wanawake katika nafasi mbalimbali za kiuongozi kwenye Serikali yake.

" Niwapongeze wanawake wa  TANESCO kwa kujitoa kwenu kuja kwenye shule hii na kuleta mahitaji yatakayowasaidia, nimesikia risala yenu kuwa mna changamoto ya Kompyuta na Vitanda kwenye Zahanati yenu ya Shule hili naahidi kulichukua na ntalipeleka kwa Viongozi wa juu naamini tutafanya kitu," Amesema Ndege.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanawake hao wa TANESCO amesema kabla ya kupeleka mahitaji hayo walifika kwanza shuleni hapo na kuuliza mahitaji wanayohitaji kwani waliona siyo vema kupeleka mahitaji ambayo pengine tayari yupo shuleni hapo na kuacha yale ambayo ni changamoto zaidi.

" Leo tumewaletea mahitaji na vifaa hivi, tunawaomba vikawe chachu kwenu ya kusoma na kuweza kufikia malengo yenu na kuja kuwa msaada kwa familia na Taifa kwa ujumla, tunahitaji kuwa na kizazi bora cha watoto wa kike watakaokuja kuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Taifa letu, " Amesema Mwenyekiti huyo.

Nae Mkuu wa Shule hiyo, Flora Nusu amewashukuru wanawake hao wa TANESCO kwa kujitoa kwao kufika shuleni hapo na kutoa misaada hiyo huku akiwaahidi kuwa itakua chachu yao ya kufanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita inayokaribia kuanza hivi karibuni.

" Huu ni moyo wa kipekee sana mmetuonesha, mngeweza kupeleka vitu hivi sehemu nyingine yeyote lakini mkaamua kuvileta kwetu, niwashukuru kwa upendo huu na hakika tutavitumia kama ambavyo nyie mmekusudia kwetu," Amesema Mwalimu Flora.
Share To:

Post A Comment: