Wanawake wanaofanya kazi  Makao Makuu yaTume ya Madini wametakiwa  kuonesha uwezo mkubwa na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pindi wanapopata fursa mbalimbali katika Taasisi mbalimbali Serikalini.


Wito huo umetolewa leo tarehe 05 Machi, 2021 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Yorkbeth Myumbilwa alipokuwa akifungua mafunzo ya wawake wa Tume ya Madini kuhusu sheria na afya  ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kinatarajiwa kuwa tarehe 08 Machi, 2021.


Amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa wanawake kwenye nafasi  za uongozi na kuwataka waliopewa nafasi hizo kuonesha uwezo wao kwa kufanya kazi kwa kuwa wabunifu na kuchapa kazi kwa bidii ili kuleta mafanikio chanya.


Katika hatua nyingine, amesema kuwa katika kutafuta usawa katika sehemu za kazi wanatakiwa kufuata sheria na taratibu badala ya kulalamika tu.


" Kwa mfano kama mtu anahitaji kupandishwa cheo kwanza anatakiwa kuangalia vigezo alivyokuwa navyo kulingana na muundo na sheria badala ya kulalamika,"amesema Myumbilwa.


Akizungumzia mafunzo hayo Myumbilwa amesema kuwa, lengo la mafunzo ni kuwapa uelewa mpana wanawake hao kuhusu masuala ya sheria na afya na kuwaandaa kuwa viongozi bora kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.


" Tunaamini kuwa ukielimisha mwanamke, umeelimisha jamii nzima, kwa kuwa ndio waangalizi wa maadili ya watoto kuanzia katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla," amesisitiza Myumbilwa.


Aidha, amepongeza wanawake wa Tume ya Madini kwa kutembelea gereza la wafungwa wanawake la Isanga lililopo jijini Dodoma na kuongeza kuwa hiyo ni ibada kamili na watabarikiwa.


Katika hatua nyingine akizungumza kwa niaba ya wanawake waliohudhuria mafunzo hayo, Afisa Ugavi wa Tume ya Madini, Jema Saria  ameushukuru uongozi wa Tume ya Madini kwa kujali Wiki ya Wanawake kwa kuwapa fursa ya kutembelea wafungwa wanawake katika gereza la Isanga na kupewa mafunzo kuhusu sheria na afya.


Ameongeza kuwa wataendelea kuchapa kazi ili kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa rasilimali za madini.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: