Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Dkt. Godbertha Kinyondo.


WAFANYAKAZI wanawake na wanaume, wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es  Salaam, watafiti wa tafiti za wajasiriamali wamesheherekea siku ya wanawake duniani kwa kufanya mdahalo kwa njia ya mtandao.

Akizungumza wakati wa kuongoza mdahalo huo  Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam Dkt.Godbertha Kinyondo alisema kuwa Mdahalo huo uliwakutanisha wanawake wabobezi katika maeneo yao ya kazi, pamoja na wanaume ili kuzungumzia mchango wa wanawake katika uchumi wa nchi, mafanikio yao, utatuzi wa changamoto wanazozikabili  pamoja na nini kifanyike ili kuendelea kuwainua wanawake katika jamii.

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ni  "wanawake na uongozi."  Amekili kuwa viongozi sio tu kwenye taasisi za serikali na kimataifa, bali, viongozi wanawake ni katika kila ngazi, kutoka katika familia, kaya, taifa, na mpaka kimataifa, kila mmoja kwa nafasi yake ya uongozi.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuwainuma wanawake wajasiriamali katika shughuli zao, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Mazana Issa alisema Baraza hilo linasaidia kuwaweka wajasiliamali katika mifumo yake ambayo inawawezesha wafanyabiashara wote wa kitanzania waweze kupata kazi kwenye miradi ya kimkakati. Aidha aliongeza kuwa, Baraza hilo  linasaidia kuwaunganisha wajasiliamali na vyombo muhimu vya serikali ambavyo vinawasaidia kuwawezesha wafanye vizuri katika biashara zao kwa ufanisi.

Mwezeshaji Dkt. Hawa Tundui, mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, amesema kupitia tafiti zilizofanyika, familia zile ambazo mwanaume anachangia sambamba na mwanamke katika uendeshaji wa biashara, biashara hizo zinafanya vizuri zaidi kuliko zile ambazo wanaume hawatoi mchango.

Amesisitiza mchango wa familia katika maendeleo ya mwanamke ni muhimu kwa maendeleo ya biashara ya familia kwa ujumla.

Na changamoto zinazoathiri biashara za wanawake katika tafiti zinazofanywa ni pale maamuzi makubwa ya biashara, yanapofanywa tu na baba, biashara inakufa. Iwapo kama mama akichukuwa sehemu kubwa ya maamuzi ya biashara, anazoshughulikia, biashara hizo zinafanya vizuri zaidi.

Mchangiaji mwingine ambaye ni Mmiliki na Mkurugenzi mwendeshaji wa Dina Flowers aliunga mkono hoja hiyo na kusema kuwa biashara nyingi za familia zinafanya vizuri zaidi kama familia imehusisha wanafamilia.

Ila ametoa angalizo kuwa wanafamilia ili wafanye vizuri katika biashara ya familia lazima wawe naujuzi halisi kulingana na biashara wanayoifanya.

Mama Bina mwenye uzoefu wa miaka 25 katika biashara hususani za maua na mboga, ameelezea alivyoanza kidogo, mpaka kiwango cha mafanikia alichofikia, na amekili kimesababishwa na ushirikiano baina yake na familia yake.

 Amesema katika familia yake watu wote, wake kwa waume, wanafanya kazi kwa pamoja iwe kuosha vyombo, kufua au kupika wanasaidia ili kumpunguzia mzigo mama yao kwani wanajua fika, kuwa anamajukumu mengi na bila wao anaonekana kuelemewa.

Kwa familia yake kufanya hivyo amesema kuwa inampa moyo, akili na miguu yake kufanya kazi zaidi.

Majukumu ya mwanamke kama mama wa familia, kama Mfanyakazi, kama mfanyabiashara na kama mwanajamii wakati mwingine inaathiri mafanikio ya biashara anayoifanya. Hivyo msaada wa wote katika familia, na nyenzo kama mashine za usafi, kufua nakadhalika ni msaada kwa akina mama.

Akijibu swali la Dkt. Kinyondo, kuhusu nini kifanyike kuhusu kutokomeza mfumo dume, mwanafunzi wa shahada ya PhD, Aloyce Gervas, alisema ni kuwafunza Watoto wakiwa wadogo kwenye familia. Amesema amekulia katika familia ya mzazi mmoja, hivyo ilibidi akafanye kazi zote za nyumbani ikiwemo kupika, kufua, kusafisha nyumba na kadhalika, kitu ambacho anakiendeleza mpaka leo, katika familia yake.

Kaimu Mwenyekiti Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), Mama Rose Nsajigwa alisema kuwa ana ushiriki wa familia yake katika biashara yake akiwa yeye ni mmliki wa kiwanda cha kuchakata mazao, jambo linalompatia mafanikio katika kazi yake.

Akielezea kazi za TWCC, alisema ina wanachama wafanyabishara wanawake zaidi ya  6,000 na wanawasaidia kupata mitaji, kuboresha kazi zao na kupata masoko. Ameongelea mshikamano mzuri walio nao, na kusaidiana katika kuendeleza biashara zao.

Kwa upande mwingine, Dkt. Kinyondo aliuliza ni jinsi gani katika mlipuko wa Covid -19 mwanawake mfanyabishara alivyoweza kufanya biashara yake, na pia kama anao wafanyakazi, je, hali yao kibiashara ilikuwaje? Utunzaji familia maana wote wako majumbani. Na alitaka kujua kama walipata msaada wo wote wa kusaidia biashara zao, na kama ni hivyo, ulitoka wapi?

Wote Mama Dina na mama Nsajigwa wakizungumzia kuhusu COVID 19, walisema kutokana na ugonjwa wa COVID 19,  vipato vilishuka, ila dawa za kiasili zimegunduliwa,  watu wameanza kula vyakula vya kuleta kinga mwilini, hii imesababisha wafanyabiashara kuingia katika kuchakata vyakula, na madawa na kuuza kwenye mitandao. COVID 19 imeibua biashara mitandaoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa (TADI), Gloria Anderson alielezea taasisi yake inavyomlenga kumpatia mtoto wa kike nyenzo za kujiami, mfano mafunzo ya tehama, ujuzi wa fedha, kuweza kutumia ujuzi huo kupata ajira au kujiajiri na kuendeleza kazi yake. Hata hivyo ameiomba serikali iboreshe sera za uwezeshaji wa vijana kufuatia na matakwa ya wakati huu.

Share To:

Post A Comment: