Sunday, 14 February 2021

WANANCHI WAOMBA MAJENGO MATATU YA KITUO CHA AFYA YAANZE KUTUMIKA

Diwani wa Kata Ijumbi, Wilbad Kakuru. Akionyesha majengo yaliojengwa
na mdau wa maendeleo, Prosper Rweyendera, na kuyakabidhi kwa Serikali
ya Kijiji hicho kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi ikiwemo huduma ya
afya.  WANANCHI Kata ya Ijumbi wilayani Muleba mkoani Kagera, wameomba majengo matatu ya Kituo cha Afya  yaliyokabidhiwa kwa Halmashauri  yaanze kutumika ili waweze kupata huduma ya matibabu kwenye kata hiyo.


Wananchi walizungumzia majengo hayo jana wakati wakieleza changamoto wanazokabiliana nazo wanapohitaji matibabu.

Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Petruinda Rwiza alisema uwepo wa kituo hicho utawaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika hospitali teule ya wilaya Rubya.

“Si hivyo tu bali itatusaidia kupata huduma za dharura hasa pale mtu anapoumwa   ghafla nyakati za usiku,” amesema Rwiza.

Akizungumzia hilo, Diwani wa Kata ya Ijumbi, Wilbard Musirigi amesema majengo matatu yalitolewa na Mfadhili Prosper Rweyendera mwaka 2019 kwa ajili ya Kituo cha Afya lakini yanahitaji ukarabati wa miundombinu ili kuyaweka katika mfumo wa Kituo cha Afya.

“Katika bajeti ya mwaka 2020/2021 Serikali ilitenga Sh milioni 50 kwa ajili ya kukarabati majengo mawili, kujenga chumba cha kuchomea taka, nyumba ya mganga na upasuaji," amesema Musirigi.

"Kwa mwaka huu ukarabati utafanyika pamoja na kukisajili Kituo, mahitaji ya huduma ya afya ni makubwa kwani kati ya Kata sita zinazokizunguka Kijiji cha Rubao ni kata moja  yenye Zahanati, kata zote zinategemea huduma kutoka kwenye Kituo hicho kikianza kutoa huduma,''amesema.

Naye, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Salehe Mruma amesema kwa sasa majengo hayo yanatumika kwa ajili ya Kliniki ya mama na mtoto.

Amesema vijiji viwili vinapata huduma hiyo Ijumbi na wananchi wengine kutoka maeneo mengine kila mwezi na watumishi wa kutoa huduma wanafika kituoni hapo kwa ratiba.

Salehe ameomba aliyewafadhi majengo asichoke kufanya hivyo kwani mahitaji bado ni mengi , baadhi ya miundombinu inaweza kuchelewa, anaweza kutusaidia hayo mahitaji ili kukamilisha haraka ukarabati.

Ofisa Mtendaji huyo amesema  alisaini mkataba wa kukabidhiwa majengo hayo pamoja na Diwani Musirigi mwaka 2019.

Amesema makabidhiano yalikuwa kati ya Prosper Rweyendera ambaye ni mmiliki wa majengo na Halmashauri ya Muleba pamoja na Halmashauri ya Kijiji cha Rubao.

Majengo hayo yenye thamani ya Sh 149,442,531 yalikabidhiwa bure kwa makubaliano kwamba yaanze kutumika kutoa huduma za afya ndani ya miaka mitatu .

Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Modest Rwakehemura akizungumzia Kituo hicho cha afya amesema ukarabati wa majengo utaanza hivi karibuni na Huduma rasmi zitaanza mwaka ujao wa fedha (2021/22).

Amesema  kwa kuanzia, kutuo kitatoa huduma za upasuaji wa dharula kwa mama wajawazito na zingine zote zinazohusu mama na mtoto.

“Tunazingatia pia mahitaji ya theater na leba (labour) kwa Huduma zaidi za upasuaji. Tutakua tukiimarisha huduma kwa awamu kulingana na bajeti inavyoruhusu.Vilevile tunashukuru kwamba wadau wengine wanajitokeza kuunga mkono juhudi za mfadhili wa kwanza aliyetupatia majengo haya matatu,”amesema. 


No comments:

Post a Comment