NA NAMNYAK KIVUYO,ARUSHA 


Mkuu wa mkoa wa Arusha Iddi Kimanta amewataka madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha kushirikiana na mkurugenzi wa jiji hilo katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kwani hali ya usafi ni mbaya katika maeneo mengi ya jiji.


Kimanta aliyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo elekezi iliyotolewa kwa madiwani wa halmashauri hiyo ambapo alisema kuwa maeneo mengi ya jiji hilo ni machafu hali inayopelekea kushusha hadhi ya jiji hivyo wahakikishe wanashirikiana ili kuhakikisha taratibu na sheria za kuliweka jiji safi zinafuatwa na watu wote.



Alieleza kuwa madiwani ndio wamebeba taswira ya jiji wakae kwa pamoja waangali wanakwama wapi katika suala la usafi kwani jiji la Arusha ni chafu, takataka zimejaa kila kona  na kutolea mfano eneo la stand kubwa hasa nyakati za usiku takataka zinakuwa zimejaa sa.


"Embu kaeni muangalie suala la usafi wa mji, tunasema ni Geneva ya Afrika lakini kwa uchafu huu hapana, takataka kila mahali  mji wetu ni mchafu jamani, hakikisheni mnapata ufumbuzi wa hili,"Alisema Kimanta.


Aidha pia aliwataka kusimamia sheria,kanuni na taratibu za halmashauri hiyo katika kuwatumikia wananchii ili kuweza  kuleta maendeleo kwa jamii hivyo wasiwe watu wa kupinga serikali katika ukusanyaji wa mapato na atayetokea kupinga asipewe nafasi.


Alisema  wasipokusanya mapato maendeleo kama miundombinu ya maji,barabara na afya  haviwezi kuendelea kwani hawapo kufurahishana bali kusimamia serikali katika kufikia malengo yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.


"Mpaka itakapofika mwezi Juni halmashauri inatakiwa iwe imekusanya billioni 22 laki hadi sasa imekusanya bilioni 6 kwa maana hii mnatakiwa kuongeza juhudi katika ujusanyaji wa mapato ili kufikia malengo haya kwani nguvu ya halmashauri ya jiji ni uwezo wake wa mapato," Alieleza.


Pia alisisitiza usimamizi wa miradi uendane na thamani halisi ya fedha kwani wananchi hawakufanya makosa kuwachagua bali walitegemea watawawakilisha vyema na kuleta maendeleo katika maeneo yao.


"Ni matarajio yangu baada ya hapa mtaanza kazi mkiwa mna uelewa wa kutosha katika kuwatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kujua mipaka yenu hivyo hakikisheni katika kata zenu mnamaliza kero ikiwa ni pamoja na kukaa katika vikao vya mabaraza ya kata na mikutano ya vijiji ili mjue shida za wananchi na kuziwasilisha katika baraza," Aliwaeleza.



Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arusha Kenani Kihongosi aliwasihi  madiwani  hao kuwana upendo na kuepuka migogoro isiyo na maana bali wasimamie mapato kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri ya jiji la Arusha.


Kenani  alisema wote kwa pamoja wanajenga nyumba moja wanatakiwa kupendana na  kufanya kazi pamoja na endapo akitokea mmoja au wawili watakaona wao ni zaidi ya wengine akiwa kama kiongozi wa wilaya hata sita kushughulika nao.


"Tupendane, tusiingie kwenye mambo ambayo yatapasua halmashauri hii, kumbukeni wakati mnaomba kura mliwaahidi nini wananchi, itakuwa ni fedhea na aibu baraza hili likiingia katika mgogoro,"Alieleza.



Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dkt John Pima alisema watahakikisha wanasimamia mapato pamoja na usafi wa mazingira huku akiwataka wananchi kutekeleza wajibu wao bila kusubiri mkono wa serikali.


"Tunaomba wananchi wazingatie sheria za mazingira kwa kutokutupa taka hovyo na wale wanaotakiwa kukusanya uchafu katika maeneo yote wakusanye kwa mujibu wa sheria lakini pia zile tozo zinazokusanywa kwa mujibu wa sheria na zenyewe zitozwe ili kuhakikisha jiji letu linakuwa safi," Alisema Dkt Pima.


Alisema kuna suala la watu kuchukua uchafu na kubeba kwenye magari yao na kuutupa barabarani  na wengine wanajua mahali pa kutupa lakini wanatupa mahali popote  jiji litawachukulia hatua za kisheria laki pia alitoa rai kuwa usafi ni afya hivyo waache kutupa taka hovyo bali wafuate taratibu na sheria za utupaji wa taka katika maeneo husika.


Meya wa jiji Hilo Maxmilian Iranqe Alisema kuwa madiwani wamejipanga kuboresha jiji la Arusha kwa kushirikiana na viongozi wote ili kuibadilisha kuwa katika hali nzuri kila sekta na kuwa na Arusha iliyo bora zaidi ya sasa.


Mmoja wa madiwani wa halmashauri hiyo Gerald John Sebastian alisema kuwa mafunzo elekezi waliyoyapata yatawasaidia kuboresha utendaji wao katika kuwatumikia wananchi wanaowawakilisha katika kusimamia maendeleo mazingira na mambo mengine yatayoleta mabadiko katika jamii.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: