Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wamekumbushwa kuzingatia maeneo muhimu ya kipaumbele yanayopaswa kutekelezwa kwenye Sekta ya Madini kama yalivyoanishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliyoisoma wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano Novemba, 2020 na Hotuba aliyoitoa Bungeni Mwaka 2015.

Hayo yamebainishwa Desemba10, 2020 na Waziri wa Madini Doto Biteko katika kikao chake na Menejimenti ya Wizara na taasisi zake, baada ya kuteuliwa na kuapishwa tena kuiongoza Wizara ya Madini.

Biteko amewataka viongozi hao kurejea tena maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 ili kuona ni namna gani masuala hayo yametekelezwa huku kila taasisi ikitakiwa kuhakikisha inayafanyia kazi maelekezo yote kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Madini inazidi kukua na kuongeza tija kwa taifa ikizingatiwa kuwa, hivi sasa sekta hiyo imeonekana kuwa kichocheo cha ukuaji kwa sekta nyingine kiuchumi.

Aidha, Waziri Biteko amesisitiza suala la ubinifu ili kuwezesha kuibuliwa kwa miradi mikubwa ambayo itapelekea kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje ya Tanzania na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye maendeleo na uchumi wa nchi.

Kadhalika, Waziri Biteko amezuia urasimu katika kushughulikia masuala yanayohusu sekta ya madini akilenga kuweka mazingira bora yatakayowezesha biashara ya madini kufanyika kwa ufanisi ili kuwezesha matokeo chanya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwemo kuwezesha uwekezaji katika sekta ya madini kufanyika bila kuwepo vikwazo visivyokuwa na sababu.

‘’ Kama kuna watu wanataka kuchimba wapewe lesni na wapewe fursa na kama kuna maoni yanayohusisha taasisi nyingine basi yafanyiwe kazi haraka. Tuwalee wawekezaji tulio nao ili waendelee kufanyakazi,’’ amesisitiza Biteko.

Ametaka kuwepo kwa mazingira wezeshi yatakayopelekea wafanyabishara na wachimbaji kufanya shughuli zaokwa amani ili kuwezesha kuzalishwa kwa ajira, teknolojia mpya za uchimbaji na uchenjuaji wa madini  vilevile, kuiwezesha sekta kuzalisha mabilionea wengi.

Vilevile, Waziri Biteko ametaka  kufanyiwa kazi suala la utoroshaji wa madini ili kuzuia mianya inayopelekea kutoroshwa kwa madini ambalo ameeleza awali lilianza kufanyiwa kazi vizuri lakini  kwa sasa tabia hiyo imeanza kurejea.

‘’ Mwanzo tulikwenda vizuri lakini sasa tabia hii imeanza kujirudia. Kwenye upande madini feki tumepambana nao na tumekamata mitandao ya watu wa madini feki,’’ amesema Biteko.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ametaka kuhuishwa kwa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ili iendane na matakwa ya sasa akirejea Marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

‘’ Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni ya muda mrefu. Sera hii ianze kuhuishwa haraka ili iandane na matakwa ya sasa kama tulivyofanya kwenye Sheria ya madini ambayo ilitoa nafasi ya kurudisha umiliki wa madini kwa wananchi,’’ amesema Waziri Biteko.

Pia, ametaka suala la kuanzishwa kwa Chama Cha Wajiolojia kupewa msukumo ili likamilishwe haraka ili kuongeza uwajibikaji wa Wataalam hao katika sekta ya madini.

Aidha, katika kikao hicho, Waziri Biteko ametumia fursa hiyo kuwashukuru watumishi wote wa wizara ya madini na taasisi zake kwa kufanya kazi kwa pamoja kama familia moja na hivyo kuwezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa  katika sekta ya madini.

‘’ Kuna wakati niliwaeleza kiu yangu ni kujengwa kwa taasisi imara. Nashukuru hata wakati sipo kila taasisi iliendelea kufanya kazi zake vizuri. Kiu yangu ni kuona wizara na taasisi zinafanya kazi kwa pamoja ili tuwatumikie watanzania na tumalize matatizo ya wadau wetu.,’’ amesema Biteko.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amempongeza Waziri Biteko kwa kuaminiwa na kuchaguliwa tena kuiongoza wizara ya madini na hivyo kutumia fursa hiyo kumkaribisha tena wizara ya madini na kueleza ‘’ mafanikio yote yaliyopatikana ni yetu sote kwani sisi sote tulioongea lugha moja,’’
.
Share To:

Post A Comment: