NA ANDREW CHALE, CHAMWINO


MBUNGE Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete ameshindwa kujizuia na kujikuta akimwaga machozi wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Kada wa Chama Cha Mapinduzi-CCM na Mjumbe wa Umoja wa Wazazi-CCM Mkoa wa Dodoma, Egla Mamoto, leo Jumanne 29, 2020 Kijijini Mpwayungu. Wilayani Chamwino ambapo zoezi hilo linafanyika.


Ridhiwani Kikwete aliungana na familia ya marehemu, marafiki, Viongozi wa vyama vya Siasa na Serikali, ndugu na jamaa pamoja na wananchi wa Kijiji hicho kumuaga mtu ambaye aligusa watu wengi wakiwemo wana CCM aliokuwa akifanya nao harakati mbalimbali za kisiasa tokea akiwa binti mdogo.


Awali msemaji wa shughuli hiyo, 'MC' alimuomba Mbunge Ridhiwani Kikwete kutoa neno na salamu za pole kwa tukio hilo hata hivyo licha ya kufika mbele ya  kipaza sauti Ridhiwani alishindwa kutoa neno la pole na kujikuta akibubujikwa machozi na uchungu huku akifuta machozi na kurejea alipokaa.


Hata hivyo, MC aliwatangazia wananchi waliofika msibani hapo kuwa, Mbunge alipokea habari za msiba wa Dada yake uliotokea leo asubuhhi wakati akiwa safarini kumzika Egla, hali iliyoibua vilio kwa upande wa akina mama waliokaa jukwaa la wageni mbalimbali pamoja na wananchi.


Ridhiwani Kikwete alisema CCM imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Egla kwani amefahamiana nae tokea 2008 katika harakati za kisiasa wakati wote wakiwa Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana Taifa-UVCCM.


"Tumeshirikiana nae kwenye harakati mbalimbali za kisiasa 2008 wakati wa kutafuta uongozi wa  Vijana Taifa alijitolea sana wakati wa Mwenyekiti akiwa Beno Malisa.


Hata baada ya kutoka UVCCM Taifa 2012, tulikuwa tukishirikiana nae

mpaka umauti unamfika hakika ni pigo kubwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Mkoa wa Dodoma na taifa kwa ujumla" Alieleza Ridhiwani Kikwete. 


Egla Mamoto alizaliwa 15/11/1983, amefariki 27/12/2020 ambapo Mwili wa Egla unaagwa  na kuzikwa leo jioni kijijini kwao Mpwayungu, Chamwino.


Mbali na Ridhiwani Kikwete, Viongozi wengine waliokuwepo ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-Utawala Bora, Deo Dejembi, Waziri wa Vijana Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Mwita, Mbunge Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde, Mwenyekiti wa UVCCM-Taifa, Kheri James pamoja na viongozi wengine mbalimbali wakiwemo wa dini.


Marehem ameacha Mme na mtoto mmoja mwenye umri wa  miaka miwili.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: