KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amemuagiza Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Kidabaga hadi bomalang’ombe  M/S BUILDERS kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa  wakati uliopangwa


Mhandisi Nyamhanga ametoa agizo hilo  leo  Disema 05,2020 kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa,

Akizungumza katika ziara hiyo amemtaka  mkandarasi huyo kutosubiri   mwezi wa nane  ufike ili kuweza kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo bali wakamilishe haraka kwa kuwa barabara hiyo ni  muhimu kwa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya  Kilolo Mkoani Iringa.

“Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, hivyo ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi ili iweze kukamilika kwa muda mfupi na viwango vinavyolingana na fedha iliyotumika” amesisitiza  Mhandisi Nyamhanga

Pamoja na hayo, amemuagiza Mkurugenzi wa Tarura Makao Makuu Mhandisi Victor Seif kufanya tathimini ya kina kuhusu ujenzi wa barabara hiyo ikilinganishwa na uzito wa magari yatakayopita ili kuweza kujenga barabara imara ambayo itahimili uzito wa mizigo itakayokuwa inapita.

“Yapo Magari yatakayosafirisha mazao mbalimbali  na mbao ni vyema tukajiridhisha  kabla ya kuendelea na ujenzi kwa kufanya mapitio ya usanifu ili barabara ziwe imara zaidi katika  kuhimili  uzito wa magari yatakayopita” Amesema Mhandisi Nyamhanga

Aidha amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanasimami kwa karibu ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kwa kuhakikisha inakamilika ndani ya muda uliopangwa kwa kuzingatia ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake Mratibu wa Tarura Mkoa wa Iringa Mhandisi Makori Kisare amesema ujenzi wa barabara ya Kidabaga – Bomalang’ombe yenye urefu wa kilometa 18.3 ni ya kiwango cha lami na itagharimu zaidi ya shilingi  bilioni 8.167

Amesema kuwa ujenzi huo umefadhiliwa na jumuiya ya ulaya chini ya program ya Agri connect ambao unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na Mufindi.

Aidha lengo la Ujenzi wa barabara hiyo ni kuwawezesha wakulima wa chai, kahawa na mbogamboga kuweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa Mkoa na taifa kwa ujumla.

Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Happiness Semeda  amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi  wa Mkoa wa Iringa na utasaidia wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.Pia amesisitiza kuwa miradi hiyo imeibuliwa na wananchi katika kutoa vipaombele vyao katika Halmashauri.

Share To:

Post A Comment: