Mgeni rasmi wa Mahafali ya 42 ya Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Sabasaba VTC Singida, ambaye pia ni Kaimu Meneja Mradi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Shanta, Elisante Kanuya, akihutubia mahafali hayo jana.
Mkuu wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Sabasaba VTC Singida, Fatma Malenga akizungumza wakati wa sherehe za mahafali hayo.
Mwanachuo aliyebobea kwenye fani ya maandishi ya Nukta Nundu, Malingira Mathias akionyesha umahiri wake kwa kuandika jina la mgeni rasmi kupitia mashine ya Braille.
Mwanachuo wa fani ya umeme majumbani, Masome Stephano, akionyesha namna alivyokidhi vigezo vya kuwa fundi wa taaluma hiyo mbele ya wageni waliofika chuoni hapo jana.
Wahitimu wakiingia kwenye viwanja vya chuo hicho kabla ya kuanza sherehe za mahafali hayo.
Wahitimu wa mahafali hayo.
Wahitimu wa mahafali hayo wakifurahia.
Wahitimu wakifuatilia matukio mbalimbali yanayoendelea.
Wageni waalikwa wakiwa kwenye picha ya pamoja .
Mwanachuo Zanura Mohamed akiwafafanulia wahitimu wenzake kupitia lugha ya alama, hususani wale wenye ulemavu wa kusikia hatua kwa hatua kuhusiana na matukio yote yaliyokuwa yakiendelea kwenye sherehe hizo.
Mhitimu wa kozi fupi fani ya mapambo chuoni hapo, Edna Alex, akipokea cheti cha kuhitimu mafunzo.
Mmoja wa wahitimu akipokea cheti cha kuhitimu mafunzo.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka mkoa wa Singida (SUWASA), Grace Lolo akilishwa kipande cha keki na mmoja wa wahitimu chuoni hapo kama shukrani kwa mamlaka hiyo kwa kuchangia shilingi laki moja kwa ajili ya shughuli ndogondogo zilizofanikisha kufanyika kwa mahafali hayo.
Katibu wa Wazazi Chama Cha Mapinduzi  mkoa wa Singida, Ibrahim Mpwapwa, akilishwa kipande cha keki na mhitimu Edna Alex, kama shukrani kwa mchango wake kukamilisha kufanyika kwa mahafali hayo.
Meneja wa Karakana ya shirika la SEMA lililopo mkoani Singida, Lameck Muyanzi, akilishwa keki na muhitimu Zanura Mohamed ambaye mafunzo yake chuoni hapo yanafadhiliwa na shirika hilo kupitia mradi ujulikanao kama YES.
Wanachuo wengine wakifuatilia sherehe za mahafali hayo.
Sherehe zikiendelea.
Sherehe zikiendelea.
Sherehe zikiendelea.
Mafunzo kwa vitendo katika mahafali hayo.
 



Na Godwin Myovela, Singida


CHUO cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Sabasaba VTC, mkoani hapa, kipo hatarini kiusalama kutokana na kukabiliwa na tatizo la kukosa uzio, hali inayoweza kusababisha wanafunzi wake ambao wengi wao ni wenye matatizo ya mtindio wa ubongo, na aina nyingine ya ulemavu kuwa katika hatari ya kupata majanga mbalimbali.

Endapo waangalizi watajisahau, au serikali kuendelea kufumbia macho changamoto hiyo, basi; kuna hatari ya wanachuo hao, hususani wale wenye mtindio wa ubongo na albino kuwa katika hatari ya kupotea, kudhurika na watu wenye nia mbaya au kupata ajali-kutokana na chuo hicho kuwa jirani na barabara ambayo hata hivyo haijawekewa matuta.

Akizungumza kwenye sherehe za  mahafali ya 42 jana, Mkuu wa chuo hicho, Fatma Malenga, aliwaomba wadau na watu wengine wenye mapenzi mema kujitokeza kusaidia kutatua changamoto zilizopo kwa muktadha chanya wa usalama wa watoto hao, wakati juhudi nyingine za serikali katika kutatua changamoto hiyo zikiendelea.

“Pamoja na mafanikio tuliyonayo, uongozi wa chuo unakabiliwa na changamoto kubwa ya ulinzi na usalama. Eneo la chuo ni kubwa lakini halina uzio,” alisema Malenga.

Changamoto nyingine zinazokikabili chuo hicho ni pamoja na upungufu wa madarasa na karakana ambazo ni kitovu cha mafunzo ya nadharia na vitendo-kwa mantiki ya kustawisha ujuzi na stadi zao katika uhalisia wa kukabiliana na teknolojia za kisasa kwenye kujiajiri au kuajiriwa, punde wanapohitimu mafunzo yao.

Kwa mujibu wa Malenga, kwa mwaka huu pekee chuo hicho kimepokea jumla ya wanachuo 228, kati yao 125 ni wanafunzi wa kozi fupi, na 103 kozi ndefu, huku idadi ya wenye ulemavu wanawake na wanaume ikifikia 60.

Mmoja wa wahitimu wa fani ya mapambo chuoni hapo, Edna Alex, aliomba pia serikali na wadau waangalie uwezekano wa kujenga haraka ukumbi kwa ajili ya sherehe na mikutano mbalimbali ya ndani ya chuo, kutokana na vijana hao mchanganyiko kukosa maeneo rasmi ya kukusanyikia na kupeana mrejesho wa mambo yao kadha wa kadha.

Awali, akitoa nasaha kwa wahitimu, mgeni rasmi wa mahafali hayo, ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Mradi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Shanta, yenye matawi yake Singida na Songwe nchini, Elisante Kanuya, aliitaka jamii kuunga mkono kwa kununua au kusaidia upatikanaji wa masoko kwa bidhaa zote za kazi za mikono zinazozalishwa chuoni hapo.

Kanuya alisema Kampuni ya Shanta kwa tawi la Singida, ambayo kwa sasa inajulikana kama ‘Singida Gold Mine inatarajia kuanza rasmi uzalishaji wake ifikapo 2022, huku akiwataka wahitimu wa chuo hicho kuhakikisha muda ukifika wanachangamkia fursa za ajira zitakazojitokeza ili kuleta ustawi wa vipato, lakini pia kuwa sehemu ya kulisaidia taifa na maono ya Rais John Magufuli katika kufikia uchumi wa juu.

“Mafunzo haya mliyopata yakawasaidie kujenga taifa, mkawe chanya na alama ya maendeleo. Tutafurahi sana kuwaona mkiwa wengi ndani ya Kampuni ya Shanta pale tutakapoanza kuzalisha ajira za kutosha,” alisema Kanuya.

Chuo hicho kinachotoa mafunzo ya ufundi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu Singida, ambacho imeelezwa huko nyuma kilijulikana kama ‘Chuo cha Wanawake Wasioona’  kilianzishwa mwaka 1977 kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania na Sweden, lengo likiwa ni kutoa huduma za marekebisho sanjari na kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata ajira na kujitegemea kiuchumi.

Hata hivyo kwa sasa kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, na kinaendelea mpaka sasa kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wenye ulemavu wa aina zote kwa gharama ya serikali. 

“Wanafunzi wanaopokelewa ni wenye umri wa miaka 15 mpaka 35 wakiwemo watumishi wa umma ambao wamepata ulemavu…huku chuo kwa sasa kikiendelea kupokea wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi, viziwi, wenye ulemavu wa viungo, wasioona na wenye tatizo la mtindio wa ubongo kwa jinsia zote,” alisema Malenga na kuongeza:

“Huduma za kimafunzo zinazotolewa chuoni hapa ni pamoja na mafunzo ya fani za ufundi wa umeme majumbani, useremala, ushonaji, maandishi ya nukta nundu, kilimo, mapishi na maarifa ya nyumbani, afya ya uzazi na stadi za kazi, ‘technical drawing’, sayansi ya kompyuta, huduma ya ushauri wa aina ya ajira na ushauri nasaha kwa wenye ulemavu hususani walioathiriwa na unyanyapaa ndani ya jamii.”

Share To:

Post A Comment: