Sunday, 22 November 2020

Mavunde azindua kisima cha maji Chikola kata ya Matumbulu Dodoma

 


 MBUNGE wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amezindua kisima cha maji katika eneo la Chikola Kata ya Matumbulu huku akiahidi kuendelea kutatua tatizo la maji kwenye jimbo lake kwa kuchimba visima vingine 20 ndani ya Jiji la Dodoma.

Kisima hicho kimechimbwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Islamic Help Tanzania kwa ushirikiano na Taasisi ya DABBAGH Welfare Trust ya nchini Denmark.

Akizindua kisima hicho, Mavunde amewahakikishia wananchi kuwa watapata huduma ya maji safi na salama ndani ya kipindi cha miaka mitano ili waondokane na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.


“Mnatumia muda mwingi kutafuta maji na kushindwa kufanya shughuli nyingine, leo nina furaha kubwa kwamba ndoto yetu ya kupata maji imekamilika,”amesema.

Amesema utekelezaji huo ni moja ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu ambapo aliahidi kutatua tatizo la maji kwa wananchi.

“Nataka ndani ya muda mfupi sana tuondoe tatizo la maji Kata nzima ya Matumbulu.Niliangalia namna ya kutafuta wadau kusaidia hili nashukuru Mungu hawa wadau wamekubali kunisaidia kutatua tatizo la maji,”amesema.

Amefafanua kuwa kisima hicho alichozindua kitanufaisha kaya 370 na wananchi zaidi ya 2000 ambapo awali walikuwa wanatembea zaidi ya kilometa nne kufuata maji.

Aidha, amesema Taasisi ya Islamic Help imeahidi kusaidia wananchi wenye mifugo ili kukuza uchumi wao.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi hiyo, Ahmed Munir, amesema Taasisi yake ipo tayari kushirikiana na wananchi wa Dodoma Mjini kupitia ofisi ya Mbunge kutatua kero ya maji kwa wananchi.

“Kwasasa tumekuja kuangalia maeneo mengi zaidi yanayohitaji huduma ya maji kwa ajili ya kuanza utekelezaji mkubwa wa uchimbaji wa visima kwenye Jimbo hili,”amesema.

Wakizungumza baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo wa maji Matumbulu, wananchi wamemshukuru Mbunge kwa jitihada zake za kutatua kero zinazowakabili ambapo walikuwa wakichota maji kwenye visima vya kienyeji vilivyochimbwa jirani na bwawa lililopo Matumbulu.

“Ni muda mrefu hakuna maji mimi nimezaliwa nimekuta hii kero, kwa kweli tunamshukuru Mbunge wetu Mavunde kwa kutuletea maji na wafadhili tumepata maji salama sasa,”amesema.

No comments:

Post a Comment