Tuesday, 6 October 2020

VIWANDA VYA MBOLEA HAPA NCHINI VINAZALISHA ASILIMIA 6 YA MAHITAJI YA WAKULIMA HUKU ASILIMIA 90 IKIAGIZWA KUTOKA NJE


NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.

Mkuu wa mkoa wa Arusha Iddy Kimanta amesikitishwa na taarifa kuwa bado viwanda vya mbolea na visaidizi vyake hapa nchini vinatengeneza asilimia 6 tu ya mahitaji ya wakulima  huku asilimia 90 zikiagizwa kutaka nje jambo ambalo amewataka watengenezaji wa mbolea na visaidizi vyake kutafuta nanma ya kuondoa changamoto zinazowakabili ili waweze kuongeza uzalishaji na matumizi ya mbolea zinazotengenezwa hapa Tanzania.

Kimanta aliyasema katika kikao kazi cha jukwaa la wawekezaji katika utegenezaji wa mbolea na vusaidizi vyake hapa nchini ambapo alisema kuwa njozi ya serikali ni kuwa na uchumi unaotegemea viwanda mojawapo ikiwa ni pamoja na viwanda vya mbolea  hivyo ni lazima wakubali kukuna vichwa kufikiria namna ya kujitosheleza kwa mbolea.

Alieleza kuwa sekta ya Kilimo ni mwajiri wa zaidi ya asilimia 60 ya watanzania, inachangia asilimia 29.1 ya pato la taifa, asilimia 30 ya pato la taifa litokanalo bidhaa za Kilimo nje ya nchi pamoja na asilimia 65 ya malighafi za viwanda vya ndani hivyo Tanzania kuishi kwa kutegemea mbolea kutoka nje kwa zaidi ya asilimia 90 ni hatari kwa nchi.

“Kama nchi ili tuweze kujitosheleza kwa bidhaa tunazotengeneza, serikali inasisitiza kuacha kuacha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa kutumia fedha nyingi za kigeni” Alieleza Kimanta

Aidha alifafanua kuwa mbolea ni chakula cha  mmea kama mimea ilivyo chakula cha binadamu hivyo maafisa ugani na watafiti waendelee kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo zingine ikiwa ni pamoja na kutumia kanuni bora za kilimo kwa kutumia njia mbalimbali yakiwemo mashamba darasa.

Sambamba na hayo pia alisema kuwa kuna dhana potofu zimekuwa zikisambazwa kuwa mbolea ni sumu inayoharibu ardhi, na mbolea zinazotengenezwa hapa nchini zina ubora duni mambo ambavyo siyo ya kweli kwani kama mbolea ikitumiwa kwa usahihi kama inavyoelekezwa na wataalamu haiwezi kuleta madhara yoyote kwa ardhi, ikiwa ni pamoja na kabla mbolea haijaruhusiwa kutumia kuna taratibu zinazofuatwa ambazo ni uchambuzi wa kisayansi, majaribio na kudhibitishwa na shirika la viwango (TBS).


Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) Profesa Anthony Manoni Mshandete alieleza kuwa Tanzania  inaendelea kutegemea mbolea kutoka nje kwa zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji ya wakulima ambapo kwa sasa ni zaidi ya tani 500,000 huku kukiwa na changamoto ya kuingizwa kwa mbolea bandia, mbolea kuchelewa kuwafikia wakulima pamoja na bei ya mbolea zinazotoka nje kuwa kubwa.

Profesa Mshandete alisema kuwa pamoja na kuboreshwa kwa mifumo ya uingizaji wa mbolea kutoka nje pamekuwepo na jitihada za wawekezaji mbalimbali kujenga viwanda vya mbolea na visaidizi vyake ambapo kwa sasa kuna zaidi ya viwanda 9 tofauti na awali kufikia mwaka 2015 kulikuwa na viwanda vinne (4) na hapakuwepo na kiwanda cha visaidizi vya mbolea.

“Pamoja na wawekezaji kujitoa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya mbolea na visaidizi vyake bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa ya nishati na malighafi na tumekutana kujadili pamoja namna ya kutatua changamoto hizi”Alisema Profesa Mshandete.

No comments:

Post a Comment