MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amepiga simu na kuwaomba wakazi wa mkoa wa Tanga wampigie kura za kutosha ili aweze kushirikiana nao katika kulijenga kikamilifu Jiji la Tanga.

 

 

“Tunataka kulijenga Jiji la Tanga kikamilifu ili mfanye biashara Kimataifa na ndio maana mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda niliamua uje Tanga. Mradi huu ni mkubwa kwa hiyo watu wa Tanga mjiandae kwa kupata fedha na ajira.”

 

 

Ameongea na wananchi hao leo (Jumapili, Oktoba 11, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Jiji la Tanga kupitia simu aliyompigia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika mtaa wa Mikanjuni kata ya Mabawa jijini Tanga.

 

 

“Mnakumbuka tulivyokuja na Rais Yoweri Museven kwa ajili ya mradi mkubwa wa bomba la mafuta? Nimemtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa aje aniwakilishe kuja kuniombea kura na kumuombea kura Waziri wangu Ummy Mwalimu pamoja na madiwani. Wana-Tanga  nawaomba kura zenu.”

 

 

“Naomba msiniangushe nileteeni Ummy Mwalimu ni mwanamama shupavu ambaye hata corona inamuogopa, huyu ni mama safi nawaomba msiende na mawazo kwamba kiongozi ni mwanaume tu kwani hata Makamu wa Rais Mama Samia ni mwanamke na anaongoza vizuri.”

 

 

Pia, Dkt. Magufuli ametumia fursa hiyo kuomba kura kwa wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa kwa sababu maendeleo hayana chama. “Naomba kura kwa watu wote wa CCM, CUF, ACT. Pia nawaomba mniletee Ummy Mwalimu na madiwani ili tuwafundishe wanaopinga maendeleo ya Tanga na wapinga mradi wa bomba la mafuta.”

 

 

Amesema Serikali inaendelea na upanuzi wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga ili ziwe bandari kubwa zaidi zitakazowawezesha kufanya biashara kimataifa, “Nahitaji nipate connection na connection kubwa ni kumchagua Ummy Mwalimu na madiwani wote wa CCM ili mipango ya maendeleo tuipange vizuri na Muheza naomba mumchague Mwana FA msinichagulie watu wanaokuja bungeni na kutoka nje.”

 

 

Kuhusu suala la fidia kwa watu waliopisha ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta, Dkt. Magufuli amesema watu wote wanaotakiwa kulipwa watalipwa na amemtuma mtendaji kutoka TPDC kwa ajili ya kufuatilia malipo hayo. “Sisi tutatekeleza kwa vitendo mambo yote yaliyomo kwenye ilani ya uchaguzi na hii ndio maana ya Hapa Kazi Tu. Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari wananchi hao wameshaanza kulipwa.

 

(mwisho)   

IMETOLEWA:

JUMAPILI, OKTOBA 11, 2020.

Share To:

Post A Comment: