Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (Mb) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel wakipata elimu ya Vipimo katika maonesho ya madini

Afisa Vipimo Bw. Lusako Mwaipaja akionesha mawe maalumu (standards) zinazotumika kuhakikia mizani ya madini.

Afisa Vipimo Bw. Lusako Mwaipaja akionesha standards zinazotumika kuhakikia mizani ya madini.

Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (Mb) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel wakipata elimu ya Vipimo katika maonesho ya madini

Afisa Vipimo Bi. Lightness Justine akitoa elimu ya vipimo katika maonesho ya madini Geita

....................................................................................................................

Wakala wa Vipimo (WMA) inawakaribisha wananchi wote wa Geita na Mikoa yote ya karibu kuhudhuria katika maonesho ya tatu ya Madini ambayo yanafanyika katika viwanja vya bomba mbili mwatulole. 

 

Lengo kubwa la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho hayo ni kuwapa elimu Wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vipimo pamoja na kuwaelezea majukumu ya Wakala wa Vipimo katika sekta mbalimbali hususani ya Madini.

Wakala wa vipimo inaishukuru sana serikali ya awamu ya tano ambayo inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanzisha masoko mbali mbali ya madini ambapo kwa mkoa wa geita kuna jumla ya masoko tisa (9) ya kuuzia na kununulia dhahabu ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa, Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale na Nyakagwe.

Akizungumza na mwandishi wetu afisa Vipimo wa Wakala wa Vipimo Geita ndugu Chrispinus Aloyce amesema kuwa, Wakala wa Vipimo inamchango mkubwa sana katika sekta ya madini ambapo biashara hiyo haiwezi kufanyika bila kuwa na mizani sahihi na iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuweza kutambua uzito halisi wa dhahabu inayonunuliwa au kuuzwa.

  Jukumu kuu la Wakala wa Vipimo katika sekta hii ni kuhakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi na pia taasisi hiyo inahakikisha inatoa ushauri wa kitaalamu juu ya mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini kwa kuwa siyo mizani yote inastahili kutumika kuuzia na kununulia madini.

Pia, ameeleza kuwa mara baada ya uhakiki wa mizani hiyo kukamilika uwekewa alama maalumu ambayo inaonesha utambuzi kuwa mizani imehakikiwa na inafaa kutumika kununulia madini.

 

 Alama zinazowekwa katika mizani iliyohakikiwa ni stika pamoja na lakiri (seal) ambayo inakuwa na alama ya nembo ya taifa pamoja na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano (20) ikiashiria imehakikiwa 2020.

Vilevile, ameeleza kuwa lengo na dhumuni la Wakala wa Vipimo kufanya uhakiki wa mizani ya kuuzia na kununulia madini ni kuhakikisha matumizi ya mizani sahihi iliyohakikiwa yanazingatiwa na kunakuwa na biashara ya usawa ambapo itawezesha Serikali kukusanya mapato kwa usahihi na wauzaji wa madini wanapata fedha stahiki kulingana na thamani ya madini wanayouza. 

 

Kadhalika, mara baada ya uhakiki wa mizani inayotumika kuuza na kununulia madini Wakala wa Vipimo hufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara katika masoko ya kuuzia madini ili kujiridhisha kama mizani bado ipo sahihi na inatumika kwa usahihi kama inavyostahili.

Wakala wa Vipimo inatoa onyo kwa wafanyabiashara kutojihusisha na vitendo vya uchezeaji wa vipimo kwa lengo la kutaka kujipatia faida zaidi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria ya Vipimo Sura na. 340 na mapitio yake mbalimbali ambayo inaeleza adhabu kwa mtu atakaye kutwa amechezea vipimo ni faini isiyopungua shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi millioni ishirini (20,000,000/=) kwa kosa. 

 Hivyo, wito umetolewa kwa watumiaji wote wa vipimo kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na wananchi kutembelea ofisi za wakala wa vipimo zilizopo katika mikoa yote Tanzania Bara kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu vipimo au kutoa maoni na kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha utoaji huduma wa taasisi hiyo.

Pia, wananchi wanakaribishwa kutumia namba ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97 endapo watakumbana na changamoto yeyote ya kivipimo na kitaalamu ili iweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: