Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa Mwaka ulioishia Mwezi Agosti ,2020 umebaki kuwa asilimia 3.3% kama ilivyokuwa kwa Mwaka ulioishia mwezi Julai ,2020.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Septemba 8,2020 jijini Dodoma,Kaimu mkurugenzi wa sensa ya watu na Takwimu za jamii Bi.Ruth Minja amesema hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa Mwaka ulioishia mwezi Agosti ,2020 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa Mwaka ulioishia mwezi Julai,2020.

“Mfumuko wa bei Kwa mwaka ulioishia Mwezi Agosti,2020 kuwa sawa na mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2020 kumechangiwa na kupungua na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Agosti,2020 zikilinganishwa na bei za Mwezi Agosti 2019”amesema.

Aidha,Bi.Minja ametaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Agosti,2020 ikilinganishwa na Agosti 2019 ni pamoja na mahindi kwa 5.8%,unga wa ngano 1.1%,mihogo 16.3% na viazi vitamu 11.9%.

Hali kadhalika baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Agosti,2020 ikilinganishwa na Agosti 2019 ni pamoja na mavazi kwa 2.2%,ada za shule za msingi na sekondari za binafsi kwa 2.4%,na huduma za malazi kwenye nyumba za wageni kwa 2.8%.

Bi.Minja ameendelea kufafanua kuwa,mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti ,2020 umepungua hadi asilimia 3.7% kutoka asilimia 3.8% kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2020.

Kuhusu hali ya Mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia Mwezi Agosti ,2020 Bi.Minja amebainisha kuwa ,nchini Kenya umebaki 4.36% huku Nchini Uganda ukipungua kidogo hadi 4.6% kutoka 4.7% kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2020.

Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu[NBS] ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa sharia ya Takwimu Sura 351 ,kwa mujibu wa sharia hiyo imepewa Mamlaka ya kutoa ,kusimamia ,kuratibu upatikanaji na usambazaji wa Takwimu Rasmi hapa nchini.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: