Na John Walter-Kiteto, Manyara.

Katika kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa mkoa wa Manyara, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilaya ya Kiteto inamshikilia Mwenyekiti wa kijiji cha Kimana Wilson Ngolanya (63) kwa tuhuma za rushwa ya ngono.
Katika taarifa iliyotolewa na Takukuru, inasema Ngalanya alikamakatwa agosti 15 mwaka huu majira ya jioni katika nyumba ya kulala wageni iliyojulikana kwa jina la Naisimo iliyoko mjini Kibaya akiwa Uchi wa mnyama na amevaa mpira tayari kwa kutekeleza uhalifu huo.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo amesema, awali walipokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji binti wa miaka 23 akimtuhumu kiongozi huyo kuomba rushwa hiyo.
"Kwa mujibu wa wa uchunguzi, Ngolanya alikuwa akiomba rushwa ya ngono ili aweze kumsaidia mlalamikaji kuwaondoa wavamizi watatu  kwenye shamba lililokuwa likimilikiwa na baba wa binti huyo ambaye kwa sasa ni Marehemu" alisema Makungu
Makungu amesema Ngolanya anafahamu kuwa shamba hilo lilikuwa la marehemu baba wa binti huyo lakini alimtaka ampe rushwa ya ngono ili aweze kuwaondoa wavamizi hao katika shamba hilo.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa binti huyo baada ya kuona usumbufu huo unazidi aliamua kutoa taarifa Takukuru ambapo baada ya kujiridhisha na uchunguzi wa awali, makachero wa Takukuru waliandaa mtego uliopelekea kukamatwa kwa mtuhumiwa katika moja ya vyumba katika nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa tayari kajiandaa kutimiza azma yake ovu.
Makungu amefafanua kuwa kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 kinasema; Mtu yeyote aliye kwenye mamlaka au uongozi ambaye kwa kutumia mamlaka au cheo alichonacho akilazimisha sharti la rushwa ya ngono ili aweze kumpa mtu yeyote ajira, kupandishwa cheo, kumpa stahiki, upendeleo au unafuu asiostahili anakuwa ametenda kosa la rushwa ya ngono na ikithibitika anastahili adhabu ya fine isiyozidi milioni tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Taasisi hiyo inatoa rai  kwa viongozi wachache ndani ya utumishi na binafsi wenye tabia au fikra kama za kuomba rushwa ya ngono waache mara moja kwa kuwa sheria ni msumeno hukata mbele na nyuma.
Pia Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu amewataka mabinti pale wanapokutana na kudaiwa rushwa ya ngono kinyume na K/F cha 25 PCCA Na. 11/2007 kama kilivyofafanuliwa hapo juu, kwamba watoe taarifa Takukuru kwa namba 113 au ofisi za Takukuru mikoa na wilaya zilizopo karibu ili kuwaondoa hao wachache wanaotumia vyeo walivyonavyo kudhalilisha utu kwa kulazimisha rushwa ya ngono.                                                                 
Share To:

Post A Comment: