Na John Walter-Manyara 
Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, imewatoza faini ya shilingi milioni 1,095,250 madereva wa malori walioshirikiana na mtumishi wa Halmashauri hiyo Joakimu Soka kukwepa ushuru wa mazao aina ya vitunguu.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara  kwa kushirikiana na jeshi la polisi waliwakamata madereva hao ambao baadhi yao ni kutoka nje ya nchi pamoja na mtumishi huyo kwa tuhuma za kula njama za kukwepa ushuru kwa kulipa fedha kidogo kuliko idadi ya magunia ya vitunguu walivyobeba na kuisababishia hasara kwa mamlaka husika.
Holle Makungu ni mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara amesema baada ya mahojiano na madereva hao, walieleza kuwa wamekuwa wakishawishiwa na watumishi wa halmashauri kupokea stakabadhi zinazoonyesha wamelipa kiasi kidogo cha fedha kinyume na uhalisia, ambapo baada ya makubaliano  hayo madereva hupewa bakshishi kidogo huku maafisa hao wakibaki na sehemu kubwa ya fedha hizo mifukoni mwao.
Makungu amesema kutokana na madereva hao kukiri makosa, walitozwa faini na kuachwa waendelee na safari kwa kuwa zao la vitunguu linaharibika mapema.
Mkuu huyo ametoa onyo kwa madereva wa malori na wafanyabiashara wenye tabia hizo waache haraka  na kwamba zoezi hilo litakuwa ni endelevu.
Amesema wakati ujao watakaokamatwa hawatapigwa faini tena kwa maana ya sheria za halmashauri  bali watashtakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi kama ilivyorekebishwa  na sheria namba 3/2016 , chini ya sheria hiyo kwa watakaothibitika kuhujumu uchumi, ambapo adhabu ni kifungo kisichopungua miaka 20 jela na  chombo kilichotumika kusafirisha na mazao yatataifishwa.     
 Makungu amemnukuu Jaji mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma ambapo Juni 17,2020 alisema  "Utashi wa kisiasa na dhamira anayoonyesha Mheshimiwa Dkt. John Magufuli haitoshi bila ya kila taasisi , kila idara na kila mwananci kukubali kwa vitendo kuwa sehemu ya vita dhidi ya Rushwa.   
Kuhusu mtumishi anaetuhumiwa kula njama hizo, ameeleza kuwa wana imani kuwa mkurugenzi wa halmashauri ambaye walishirikiana naye katika zoezi la ukamataji katika kijiji cha Kitimachungu kilichopo mpakani mwa Simanjiro na wilaya ya Mwanga, atachukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya mtumishi huyo Joakimu Soka kabla Takukuru haijamfikisha Mahakamani.
Aidha amesema hilo litakuwa ni fundisho kwa watumishi wachache wanaoihujumu halmashauri ya Simanjiro na wote wenye mawazo ya kuhujumu mapato ya halamashauri  ya Simanjiro kama mtumishi huyo.         
Share To:

Post A Comment: