Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia) akitoa maagizo kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini Rea awamu ya pili Mkoa wa Singida pamoja na Shirika la umeme Tanzania Tanesco Mkoa huo kuhakikisha wanamaliza mradi huo ifikapo Septemba 10 mwaka huu.

 Ziara ya Waziri Kalemani ikiendelea.
Mafundi wakiwa kzini.




Na Ismaily Luhamba. Singida.

WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini Rea awamu ya pili Mkoa wa Singida pamoja na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa huo kuhakikisha wanamaliza mradi huo ifikapo Septemba 10 mwaka huu.

Ametoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi baada ya kutembelea Kijiji cha Kisiriri kilichopo Wilayani Iramba Mkoni hapa ambapo alikagua na kujionea kazi ya kusambaza umeme wa REA awamu ya pili ambapo inafanyika kwa kusuasua.

Dkt. Kalemani akaitaka kampuni ya JV MEMEC &DESCO ya kitanzani inayotekeleza Mradi huo kuwa ifikapo septemba 10 mwaka huu wawe wamekamilisha mradi huo.

“Nasema hivi kuanzia leo hakuna mtu kurudi mjini hasa nyinyi wakandarasi mtabaki huku mpaka tarehe 10 nitakapo kuja mimi mwenyewe kwenye uzinduzi na uwashwaji umeme katika vijiji vyote 51 ili kumaliza huu mgogoro, nawataka hawa wakandarasi Tanesco pamoja na REA wawe wanakwenda kusaini kila siku katika kituo cha Polisi kilichopo karibu na sehemu wanayo fanyia kazi na mimi niwe napatiwa taarifa kila wiki” alisema Kalemani. 

Pia Kalemani amewataka Tanesco kuipima Kampuni ya JV EMEC & DESCO kwa siku saba kama kweli wanaweza kumaliza kazi hiyo kwa muda aliyowapa, na kama hawawezi kumaliza kwa wakati wavunje huo mkataba na kampuni hiyo.

Aidha ameipongeza kampuni ya CCCE ETERN CONSORTIUM LTD  ya kichina ambayo inatekeleza mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza kwa kufanikiwa kusambaza umeme kwenye Vijiji 1680, ambapo vimebaki  vijiji 26 kwa mkoa mzima ili kumaliza kazi ya kusambaza umeme.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi amesema atahakikisha anasimamia maelekezo hayo ili kabla ya muda uliopangwa na Waziri kuisha mradi huo uwe umekamilika.

“Kupitia kamati yangu ya ulizi na usalama nitahakikisha mkandarasi anakwenda kituo cha polisi kila siku na kusaini kama ulivyoagiza na ripoti hiyo nitakutumia mimi mwenyewe.” alisema Dkt. Nchimbi.

Katika hatua nyingine Kalemani amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Rea awamu ya pili kutakiwa kuripoti kituo cha polisi kila siku mpaka hapo watakapo maliza kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji 51 mkoani Singida.
Share To:

Post A Comment: