Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, Justin Nyari akizungumza na wamiliki wa migodi ya Tanzanite kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Kazamoyo kwa Luka Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro jana.


Na Mwandishi Wetu,  Manyara

MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoani Manyara, Justin Nyari amesema watamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu mbunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Millya (CCM) aliyemaliza muda wake kutokana na namna alivyokuwa anawatetea Bungeni wachimbaji madini ya Tanzanite.

Nyari aliyasema hayo jana mji mdogo wa Mirerani kwenye kikao cha wachimbaji wa madini ya Tanzanite cha kujadili mikakati mbalimbali ya uchimbaji ikiwemo usalama migodini na kuchangia chama hicho.

Alisema wachimbaji madini wa mkoa huo wanatambua jitihada za dhati za Ole Millya alipokuwa anawatetea bungeni hivyo ili kurudisha fadhila kwake watamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 25 mwaka huu.

Alisema wanatambua vikwazo mbalimbali alivyokuwa anavipata Ole Millya lakini alisimama kwa miguu miwili na wachimbaji wadogo wa madini hivyo watahakikisha wanamuunga mkono ili arudi bungeni kuendelea kuwatetea.

 "Mchezaji mahiri ni yule ambaye anacheza vizuri uwanjani na anasaidia timu kupata ushindi hivyo hatuna sababu ya kuchagua mbunge mwingine ili hali huyu tuliyekuwa naye alikuwa anatusaidia sisi wachimbaji madini," alisema Nyari.  

Alisema wachimbaji madini wanatambua kuwa Ole Millya alikuwa halali usingizi pindi wakimshirikisha matatizo mbalimbali ya wachimbaji madini hivyo cha kumlipa ni kuhakikisha wanaendelea kumuunga mkono ili achaguliwe tena kuongoza jimbo hilo.

Kaimu ofisa madini mkazi wa Mirerani, Hamis Kamando alisema Ole Millya ni kiongozi makini kwani walifanya kazi mbalimbali wakati mbunge huyo akiwa mjumbe wa kamati ya bunge ya nishati na madini.

"Waziri wa madini Dotto Biteto, Naibu waziri Stanslaus Nyongo na mbunge wa jimbo la Simanjiro Ole Millya nawaombea washinde uchaguzi wao kwani ni viongozi mahiri wenye uzalendo wanaotanguliza mbele maslahi ya Taifa,״ alisema Kamando.

Kwa upande wake, Ole Millya alisema anashukuru namna wachimbaji madini walivyoshirikiana naye wakati akiwa bungeni na kuhakikisha wanapata haki zao na ataendelea kuwa nao kwani ana imani kubwa atachaguliwa tena kuwa mbunge wa jimbo la Simanjiro.

"Namshukuru kila mchimbaji niliyeshirikiana naye katika kutetea wachimbaji wadogo ikiwemo Marema, Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Adam Kobelo na Mwenyekiti wa Tamida Sammy Mollel kwa kweli tulipambana,״ alisema Ole Millya.

Alisema anampongeza Rais John Magufuli kwa namna anavyowajali wanyonge hasa wachimbaji wadogo kwani alipojenga ukuta kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi baadhi walichukia hilo lakini kutokana na mafanikio yanayopatikana wote wamekubali.
Share To:

Post A Comment: