Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Benki ya NMB - Eunice Chiume, akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari katika Banda la NMB lililopo viwanja vya Saba Saba.
Wafanyakazi wa Benki ya NMB katika picha ya pamoja ndani ya Banda la NMB - Saba Saba, baada ya mkutano na waandishi wa habari.
 


Kwa mara nyingine tena, Benki ya NMB inashiriki maonesho ya Saba Saba ambayo mwaka huu yameanza rasmi tarehe 01/07/2020 ikiwa na malengo zaidi ya kutangaza bidhaa na huduma zake mbalimbali, lakini pia kuunga Mkono kaulimbiu “Uchumi wa viwanda kwa ajira na biashara Endelevu”

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Benki hiyo - Eunice Chiume, amesema  Benki ya NMB inashiriki kimkakati zaidi, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kibenki zikiwemo kuweka na kutoa pesa/ kubadilisha fedha hata za kigeni, kuwahamasisha na kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa huduma za kibenki na shughuli za kifedha katika maendeleo ya mtu binafsi, taasisi na taifa kwa ujumla.

“Kwa ufupi, tunaweza kusema kuwa Benki ya NMB imehamia Saba Saba kwani huduma zetu zote za kibenki na nyingine mbalimbali zinapatikana kwenye banda letu. Kuwepo kwetu hapa ni zaidi ya kujitangaza kwani pia tunataka kuwaonyesha Watanzania jinsi huduma zetu mbalimbali zikiwemo zile mpya kama za bima zinavyochangia kwenye ukuaji wa uchumi” Bi. Eunice Alisema.

Katika kusogeza huduma zake karibu na wateja wake na wote wanaotembelea maonesho hayo, NMB ina zaidi ya mawakala 20 waliotapakaa sehemu mbalimbali za viwanja vya Saba Saba pamoja na mashine za ATM. Huduma nyingine zinazopatikana ni kufungua akaunti mbalimbali kama vile za watoto, Pamoja, Chap Chap na Fanikiwa.

Huduma zingine ni kama Bima ‘NMB Bancassuarance’ ambayo ina faida nyingi na rahisi sana kwani NMB inashirikiana na kampuni kubwa za bima ambazo kwa pamoja wameweza kutoa viwango shindani vya mikataba mbalimbali ya bima kama vile, maisha, afya, moto, magari, nyumba na nyingine nyingi.

Bila kusahau huduma za kilimo biashara ‘Agri Business’ ambako Benki ya NMB ina wataalamu kwa ajili ya kutoa elimu ya mikopo na kuonyesha jinsi ya kuongeza faida na manufaa kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Vile vile, watalaamu wa kukuelimisha masuala ya kumiliki nyumba “NMB Mortgage” nao pia wapo kutoa elimu bila kusahau ‘Wajibu Corner’ kwa ajili ya kutoa elimu ya masuala ya fedha na benki kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 19 ikilenga kwenye masuala ya umuhimu wa kuwa na akiba kwa ajili ya maisha ya baadae.

Tembelea Banda la NMB lililopo kwenye makutano ya Mtaa wa Mabalozi na Carnivore, namba 24C pembeni ya banda la SIDO ufurahie huduma zao.
Share To:

Post A Comment: