Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe

Ili kukabiliana na changamoto ya uuzaji wa mazao mbalimbali ya wakulima nchini katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona serikali imetangaza na mifumo mitatu ya uuzaji wa kahawa.

Mifumo hiyo ni uuzaji wa kahawa kwa soko la moja kwa moja (Direct Selling), Mfumo wa kuuza kupitia minada ambapo vyama vya ushirika vitakusanya mazao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na mfumo wa tatu ni wakulima kuingia makubaliano na wamiliki wa viwanda vya ndani ya nchi vya uchakataji wa kahawa ili kuwauzia kahawa yao.

Serikali imewataka wakulima kutumia fursa hiyo ya uuzaji wa kahawa kwenye maeneo watakayoona kuna wanunuzi wenye bei nzuri lakini wauzaji hao wasiende moja kwa moja kwa wakulima badala yake wanunue kahawa kupitia kwenye vyama vya Ushirika.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 9 Juni 2020 wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya Kahawa Wilayani Mbozi Mkoani Songwe uliofanyika katika ukumbi wa kanisa la Moravian Sala-Ichenjezya.

Amesema kuwa serikali haiwezi kuzuia wanunuzi binafsi kwani biashara ya mazao na bidhaa zingine ni muhimu kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi hivyo hivyo ushindani ni muhimu ili kuimarisha bei ya mazao ya wakulima.

Waziri Hasunga amesema kuwa serikali inazo taarifa za kutosha juu ya Afisa Ushirika wa Wilaya ya Mbozi Ndg Fredy Katoto kuihujumu serikali kwa kutotekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi mbalimbali hivyo serikali itamchukulia hatua kali za kisheria mtumishi huyo kwani anawapotosha wakulima.

“Mtumishi wa Umma ambaye umeajiriwa unawadanganya wakulima, na wewe ndiye umekuwa tatizo kwenye kilimo chetu mnakaa huko mnapanga namna ya kulipa lakini hamlipi kwa maelekezo ya serikali taarifa tunazo, Kuna wakulima mpaka sasa hivi hawajalipwa fedha zao kwa sababu ya Katoto huyu nitamshughulikia” Alikaririwa Waziri Hasunga

Mhe Hasunga ameongeza kuwa hakuna Marais wawili katika nchi hii badala yake kuna Rais mmoja wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ambaye akitoa maagizo watumishi wengine wote wanapaswa kufuatwa na hawatakiwi kutoa maagizo mengine yoyote zaidi ya utekelezaji.

“Mimi ndio nimepewa mamlaka (Instument) inayoniambia natakiwa kutoa maelekezo ya namna ya kukisimamia kilimo nchini, Vyama vya Ushirika ni wanunuzi kama wanunuzi wengine kazi yenu ni kukusanya na kutafuta soko la mazao hivyo sitarajii kutoa maelekezo halafu kuna mtu ayapinge tena Mtumishi wa Umma” Amesema Mhe Hasunga

Katika usimamizi madhubuti wa sekta ya Ushirika nchini, Waziri wa Kilimo Mhe Hasunga amesema kuwa ili kudhibiti wizi na ubadhilifu kwenye vyama vya Ushirika unaojitokeza mara kwa mara serikali imeamua kuja na mkakati wa kuwaajiri Mameneja wa vyama hivyo ili kusimamia na kudhibiti mali na fedha zote za wakulima.

Akizungumza kwa niaba ya wanunuzi binafsi wa kahawa Ndg Tikson Nzuda amesema kuwa wanunuzi hao wana fedha za kutosha za kununua kahawa yote ya wakulima hivyo wameiomba serikali kuwapatia leseni haraka iwezekanavyo ili waingie sokoni.

Ameongeza kuwa wanunuzi binafsi tayari wamekopa fedha kwenye Taasisi mbalimbali za kifedha zikiwemo benki lakini mpaka sasa hawajapewa kibali jambo ambalo ni hatari kwao katika mikopo hiyo.

Share To:

Post A Comment: