Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amefungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC na kuzitaka nchi wanachama kushirikiana na kuchukua hatua zinazotekelezeka katika kukabiliana na madhara yatokanayo na mlipuko wa janga la Virusi vya Corona.

Amesema changamoto zitokanazo na ugonjwa wa COVID 19 zipo wazi na zinazikabili nchi zote hivyo hazina budi kuungana na kutafuta suluhisho la pamoja ili  kunusuru uchumi na athari nyingine za kijamii.

Prof. Kabudi amesema ili kupata suluhisho la kudumu dhidi ya janga hilo Nchi za SADC  ni vyema zikashirikiana na Jumuiya nyingine za kikanda kama EAC na COMESA ili kuwa na miongozo na viwango vya pamoja katika kuendesha shughuli za usafirishaji wa binadamu, bidhaa na huduma huku hatua za kujikinga zikuichukuliwa.

Amesema ni muhimu kwa nchi za SADC  kuzingatia miongozo ya wataalamu wa afya wakati zikiendesha biashara na usafirishaji wa bidhaa na huduma ili kulinda uchumi na kuondoa umasikini huku zikikabiliana na ueneaji wa janga la Corona.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri umejadili utekelezaji wa maazimio ya Baraza la Mawaziri dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa COVID 19, kupokea taarifa ya Mkutano wa Kamati ya Wataalamu ya SADC ya kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC uliofanyika tarehe 05 Juni 2020 na upendeleo utakaotolewa na India kwa nchi za SADC zitakaponunua dawa, vifaa kinga na vifaa tiba kwa ajili ya COVID 19.

Mkutano pia umepitia na kujadili Mwongozo wa Kikanda wa Urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji wa shughuli za usafirishaji ndani ya SADC pamoja na masuala ya uratibu, usimamizi na uangalizi wa usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia, ukaguzi dhidi ya Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya kuendeleza shughuli za biashara wakati huu wa janga la CORONA ili kunusuru uchumi na kupunguza umasikini ndani ya jumuiya.

Mkutano huo umekutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Share To:

Post A Comment: