Na John Walter-Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, imemfikisha kwenye Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mirerani, Yesaya Songelaeli Yindi kwa makosa ya rushwa.

Taarifa iliyotolewa  na Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, Juni 9 mwaka huu, imeeleza kuwa Songelaeli ameshtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa ya shilingi 407,000 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefred Myenzi.

Makungu alisema katika kesi hiyo namba 47/2020 Songelaeli ameshtakiwa kwa kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1) (b) na 15 (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

Alisema katika kesi hiyo iliyopo mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya hiyo, Charles Uiso na wakili wa TAKUKURU, Adam Kilongozi, mfanyabiashara mwingine Antipas Benedict Ngelesh aliunganishwa kwenye kesi hiyo.

Alisema uchunguzi wa TAKUKURU wilayani Simanjiro ulibaini kuwa Mkurugenzi Myenzi alitoa maelekezo ya kubomolewa kwa kibanda cha kuoshea magari cha Ngelesh kilichojengwa kinyume na utaratibu katika eneo la kitega uchumi Mirerani.

"Songelaeli akiwa ni Mwenyekiti wa wa wafanyabiashara wa eneo hilo mwenye ushawishi mkubwa alichukua fedha hizo za rushwa na kuzituma kwa Mkurugenzi ili amshawishi abadili uamuzi wa kuvunja kibanda hicho," alisema Makungu.

Hata hivyo, washtakiwa hao Songelaeli na Ngelesh wamekana mashtaka dhidi yao na wapo nje kwa dhamana na kesi hiyo itaendelea mahakamani hapo Julai 02 kwa usikilizaji wa awali.
Share To:

Post A Comment: