Na. Majid Abdulkarim

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo amemtaka Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Pwani Dkt. Delphine Magere kuanza utendaji kazi wake kwa kufanyia kazi  miradi ya mabweni, mabwalo na vituo vya afya ambavyo havijakamilika kwa wakati kwani ni miradi iliyotumia pesa nyingi na muda mrefu katika Mkoa huo.

Mhe. Jafo ametoa kauli hiyo leo wakati Dkt. Magere alipokuja kuripoti OR-TAMISEMI Mtumba Jijini Dodoma mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kukabidhiwa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na Kitabu cha Bajeti 2020/21, Mafanikio ya Miaka Minne ya OR-TAMISEMI,Sheria ya Tawala za Mikoa pamoja na nyaraka zingine mbalimbali.

Akizungumza Mhe. Jafo amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kufanya ujenzi na maboresho katika sekta ya Elimu na Afya Mkoani pwani na baadhi ya Halmashauri zingine hazifanyi vizuri katika usimamizi wa miradi hiyo.

“Dkt.Magere hakikisha unasimamia mabweni, mabwalo, vituo vya afya na Hospital za Wilaya ambazo zinaendelea kujengwa na kukarabatiwa, kazi hiyo ifanyika kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa, hakikisha force account inatumika katika miradi hiyo na inakamilika kwa wakati”, ameelekeza Mhe.Jafo.

Aidha Mhe. Jafo amemtaka Dkt. Magere akasimamie ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo kwa kuwa vimeshafika kwenye Ofisi za Mamalaka ya Mapato ya Mikoa na vinatakiwa kuwafikia walengwa haraka iwezekanavyo.

Halkadhalika alisisitiza Dkt. Magere kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri zote na kuhakikisha fedha hizo  zinatumika kwa kuzingatia taratibu sahihi.

“Ukusanyaji wa mapato uzingatia matumizi ya mashine za kieletroniki ili kusaidia kupunguza upotevu wa fedha za Serikali na kuongeza mapato ya halmashauri ili ziweze kujiendesha na kutekeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea Ruzuku toka Serikali kuu na kwa wafadhili” alisema Jafo.

Mhe. Jafo alimalizia kwa kumsisitiza Dkt. Magere  kusimamia nidhamu ya watumishi, matumizi mazuri ya rasilima za taifa na uwajibikaji ili kuleta utendaji mzuri katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Pwani.

Naye Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamuhanga amempongeza Dkt. Magere kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na kumtaka kuchapa kazi ili kuleta matokeo chanya kwa Mkoa wa Pwani.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Dkt. Delphine Magere amesema kuwa anamshukuru  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa nafasi hii na amekwishakuanza  kazi hata kabla ya kuapishwa kwa kutembelea Wilaya 6 na Halmashauri 7 za Mkoa wa Pwani.

“Nazidi kuwaomba wananchi na watumishi wote wa Mkoa wa Pwani tushirikiane katika kuchapa kazi ili kuleta maendeleo katika mkoa wa Pwani na Taifa kwa Ujumla” alisema Dkt. Magere.

MWISHO
Share To:

Post A Comment: