Na John Walter- Manyara.
Mahakama  kuu ya Tanzania kanda ya Arusha imemhukumu kifungo cha miaka 7 gerezeni  aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya wilaya Simanjiro Mkoani Manyara, Peter John Mollel kwa makosa ya wizi akiwa mtumishi wa umma.
 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 8, 2020, kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara,Holle Makungu  amesema kwamba hukumu hiyo ilitolewa mei 7 mwaka huu (2020) na Naibu Msajili wa mahakama kuu ya kanda ya Arusha,John Mkwabi.
Kamanda huyo wa TAKUKURU alisema kwamba pamoja na adhabu hiyo iliyotokana na makosa 11 ya wizi yaliyofanywa na mshatakiwa akiwa mtumishi wa umma, Hakimu Mkwabi pia alitoa adhabu ya kulipa faini ya shilingi milioni  4,000,000  kwa  kila kosa  kwa  makosa 9 ya matumizi ya nyaraka  kumdanganya mwajiri, sawa na shilingi milioni 36,000,000  au kifungo cha miaka mitatu jela.
Hakimu Mkwabi pia alimhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha mwaka mmoja gerezani bila faini kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.
Adhabu hiyo iliotolewa mei 7 mwaka huu na hakimu Mkwabi,  katika kesi ya jinai Namba CC.48/2016 aliyokuwa akiisikiliza katika mahakama ya Wilaya ya Simanjiro -Orkesumeti Mkoani Manyara.
Makungu alisema mwingine aliyetiwa hatiani katika kesi hiyo na kupewa adhabu sawasawa na mshtakiwa wa kwanza ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo  Ester Melkior ambaye alikuwa mhasibu msaidizi katika Halmashauri hiyo ambapo washtakiwa wote wawili wamepelekwa Gerezani kuanza kutumikia kifungo.
Awali  waendesha mshataka wa TAKUKURU Isdory Kyando akisaidiwa na Adamu Kilongozi waliwafikisha washtakiwa hao mahakamani hapo na kuwasomea jumla ya makosa (24),katika makosa hayo (10) yalihusu kutumia nyaraka za kumdanganya mwajiri kinyume cha cha kifungo cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  namba 11/2007.
"makosa mawili yalihusu matumizi mabaya ya madaraka kifungu cha 31 sheria ya kuzia na kupambana na rushwa namba 11/2007 na makosa 12 yalihusu  wizi uliofanywa na washatakiwa wakiwa watumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258 na 270 vya sheria ya kanuni ya adhabu"Alisema Makungu
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Manyara Holle Makungu aliendela kueleza kwamba, waendesha mashata hao waliwasilisha ushahidi usioacha shaka mahakamani hapo kuonyesha kwamba kati ya mwaka 2008 na 2010 mshatakiwa wa kwanza kwa nafasi yake ya mweka hazina wa Halmashauri alikuwa ndiye muidhinishaji wa nyaraka hizo na mshatakiwa wa pili kwa nafasi yake ya mhasibu Msaidizi ndiye aliyeandaa nyaraka hizo.
"Kwa pamoja walishirikiana kuzidisha orodha ya walipwaji na kiasi cha mishahara ambacho walipaswa kulipwa kwenye hati za malipo kisha kuziwasilisha nyaraka hizo benki kwa ajili ya malipo ambapo fedha hizo zilizokuwa zikizidi zilikuwa zinaingizwa kwenye akaunti za benki za washtakiwa na kisha washtakiwa hao kuzitumia kwa manufaa yao,hivyo jumla ya fedha walizojipatia kutokana na udanganyifu huo ni sh.Mil.34,520,000 "alisema Makungu.
Aidha alisema  kabla ya adhabu hiyo kutolewa na Hakimu Mkwabi,wakili wa utetezi Justus IIyarugo aliiomba mahakama iwapunguzie adhabu washtakiwa kwa kuwa mshtakiwa Peter John Mollel ni baba mwenye familia inayomtegemea, pia wakili huyo aliiomba mahakama imuonee huruma na kumpunguzia adhabu mshtakiwa wa pili Esta Melkior kwa kuwa ni mama  mwenye mtoto mmoja ,hana mume pia ni mlezi wa mama yake mzazi.
Alisema  Holle Makungu kwamba kwa upande wa waendesha mashtaka wa TAKUKURU waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa  kwa kuwa makosa waliyoyatenda ya rushwa na wizi wakiwa watumishi wa umma ni kati ya makosa mabaya na ndiyo maana bunge la Tanzania liliweka adhabu kali kwa makosa hayo ili iwe fundisho kwa watumishi wa umma wenye fikira za wizi na rushwa katika utumishi wa umma.
Hata hivyo Hakimu wa Mahakama hiyo ya Tanzania kanda ya Arusha John Mkwabi baada ya kusikiliza na kuzingatia hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka na upande wa utetezi aliweza kutoka adhabu kwa mjibu wa sheria kulingana na makosa ambayo washtakiwa waliyatenda .
Hata hivyo, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara,Holle Makungu alitoa wito kwa watumishi wa umma kuridhika na vipato vya haki wanayolipwa na Serikali na kwa wale ambao wanafikra za kufanya wizi wakiwa watumishi wa umma ,ubadhirifu,ufisadi na rushwa hawatakuwa salama .


Share To:

msumbanews

Post A Comment: