Na Allawi Kaboyo-Muleba





Kufatia kuwepo kwa vitendo vya uvuvi Haramu katika ziwa Victoria,Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco  Gaguti amekabidhi boti tatu mpya  kwa watendaji wa Kata za Bumbire na Ikuza na boti moja kubwa kwa sekta ya uvuvi kwa lengo la kudhibiti uvuvi haramu wilayani Muleba.
Zoezi hilo lilifanyika katika kijiji cha Katembe Kata Nyakabango wilayani Muleba ambapo mkuu huyo aliipongeza halmashaurihiyo kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kuhakikisha serikali inaendelea kupata mapato hasa kupitia uvuvi na kuzitaka halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
“Naipongeza sana Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kwa utekelezaji mzuri wa shughuli za maendeleo hususani ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo kwa miaka 3 mfululizo imeongoza kwa ukusanyaji mapato uliovuka malengo ya mwaka kwa mkoa wa Kagera, na hapa nitoe malekezo mahususi kwa harmashauri nyingine kuiga mfano huu.” alieleza Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti.
Gaguti amewataka watendaji waliokabithiwa boti hizo kuhakikisha wanazifanyia kazi iliyokusudiwa na kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi maana hakuna tena visingizio vya kwenda kuwahudumia wananchi kwa kigezo cha usafiri, na kuwasihi kutozitumia kama fimbo ya kuwanyanyasa wananchi badala ya kuwahudumia.
Aidha, amewasihi wananchi kuanza kujishughulisha na uvuvi wa kisasa kwa kuwa na vikundi vitakavyowawezesha kupata fedha kutoka taasisi za kifedha Pia watumie zana za kisasa na kuwa malengo ya kufanya uvuvi wa kibiashara hata kwa nje ya nchi na kueleza kuwa mkoa umejipanga kuleta wawekezaji watakaowekeza katika sekta ya uvuvi.
“Tunatakiwa kujua kuwa Mkoa wa Kagera ni mkoa wa kimkakati kwa maendeleo ya nchi, sisi kama Serikali ya mkoa tunao mpango wa kuwaleta wawekezaji watakao wekeza katika sekta ya uvuvi hivyo ni wasihi wananchi na wavuvi tufanye uvuvi wa tija wenye kufata taratibu zote kwa kutumia nyezo zinazoruhusiwa, tutakuwa waajabu kama tutawaleta wawekezaji na tukakutwa sisi wazawa ndo sababu ya kubwa ya kuendeleza uvuvi haramu katika ziwa letu.” Alisisitiza Gaguti.
Akisoma taarifa kwa mkuu wa mkoa, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bw.Emanuel Shelembi alisema kuwa upatikanaji wa boti hizo utasaidia ufanisi katika utendaji kwenye visiwa hivyo ikiwemo kuthibiti uvuvi haramu, kuthibiti utoroshwaji wa mazao ya samaki, kusaidia ufatiliaji wa mapato pamoja na kurahisisha usafiri kwa watumishi waishio visiwani.
“Upatikanaji wa boti hizi tatu unafanya kuwa na jumla ya boti nne zilizonunuliwa katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ikiwemo boti iliyonunuliwa katika kipindi cha 2018/2019, hata hivyo boti hizi unazozikabithi zote zimenunuliwa zikiwa na vifaa vyote vya usalama na uokoaji kama vili life jacket 38 na maboya matatu kwa kila boti ambavyo vitatumika wakati wote chombo kitakapokuwa majini.” Alisema Shelembi
Kwaupande wao watendaji waliokabithiwa boti hizo wameishukuru serikali kwa kuwajali na kuwapatia usafiri na kueleza kuwa wamekuwa wakitaabika hasa nyakati za usiku kufanya doria na kazi mbalimbali katika visiwa hivyo suala lililokuwa likipelekea kuhatarisha maisha yao nap engine doria kutofanikiwa kutokana na kutumia boti za wavuvi.
Boti hizo zimenunuliwa kwa fedha za mapato ya ndani ambapo boti kubwa imegharimu Tsh. 103,887,534.00 na boti mbili ndogo kila moja imegharimu Tsh. 34,789,780.00 na zote zimekabithiwa kwa wahusika ambapo Boti kubwa ina injini mbili zenye nguvu ya (Horse Power) HP 85 kila injini moja ina uwezo wa kubeba watu 16-18. Na boti mbili ndogo zenye injini moja moja kila injini ina nguvu ya (Horse Power) HP 40 kila moja ina uwezo wa kubeba watu 8-12.
Share To:

Post A Comment: