Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Chama cha    waandishi wa Habari kanda ya kati ,Cetral Press Club[CPC]kimefanya uchaguzi na kupata viongozi wapya  kwa kipindi cha miaka 5.

Akitangaza matokeo hayo  jijini Dodoma ,Mwenyekiti  wa Uchaguzi   huo ,Abubakari Famau ,Mwakilishi wa Shirika la utangazaji Uingereza [BBC] amesema mwenyekiti mpya ni Mussa Yusufu kutoka Uhuru Media,huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikichukuliwa na Mbashiru Katare kutoka Kampuni ya Magazeti Ya Serikali TSN.

Katibu mkuu mpya  katika chama cha klabu ya waandishi  wa Habari  kanda ya kati [CPC]ni Benchine Bango mwandishi wa kujitegemea na katibu Msaidizi Musa Enock kutoka Afm Radio huku nafasi ya wajumbe ikichukuliwa na watu  watatu ambao ni Jasmine Shamwepu  kutoka ABM radio,Doto Kwilasa kutoka gazeti la jamvi la Habari pamoja na Amani Mbando kutoka Channel Ten.

Naye Mwenyekiti Mteule  wa CPC  Mussa Yusuph amesema”Kwanza kabisa natoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa rehema aliyetujaalia sote kwa pamoja kujumuika kwenye mchakato mzima wa uchaguzi kisha kutuvusha tukiwa na amani, umoja, furaha na upendo.

Pili, shukrani zangu za kipekee kwenu wanachama wenzangu kwa imani kubwa mlioionyesha kwetu wagombea wote watatu, mimi, Magnus Mahenge na Daniel Mkate, hakika naimani mmetuamini sana kama ilivyojidhihirisha imani yenu kwenye mchakato mzima wa kur zilizopigwa.

Kwa dhati ya moyo wangu wagombea wenzangu, Magnus Mahenge na Daniel Mkate, ni kaka zangu wa karibu na nimejifunza na nitaendelea kujifunza mengi kutoka kwao, hivyo basi naahidi kuendelea kuchota busara na mawazo yao mazuri kwa mustakabali wa maendeleo ya CPC.

Ndugu wanachama wenzangu, imani yenu kubwa mlioionyesha kwangu, hilo ni deni ambalo ninapaswa kulilipa iwe kwa jasho, damu, machozi, mchana au usiku lazima niwatumikie kwani mimi kwenu sio kiongozi bali mtumishi wenu ninayepaswa kuwatumikia.

Yapo mengi niliyoahidi na zipo ahadi zingine za viongozi wenzangu wateule, zote kwa pamoja lazima tuzitimize pasi na ubabaifu wa aina yeyote, hivyo basi viongozi wenzangu nao wanapaswa kufahamu deni tunalopaswa kulilipa na tunapaswa kufahamu CPC sio mahali pa kuvimbisha matumbo yetu.

Jukumu letu kubwa ni kurejesha imani kwa wanachama, kukifanya chama kiwe mikononi mwa wanachama, wanachama wajivunie na kile tutakachokitekeleza na kamwe viongozi tusigeuke magwiji wa kujimwambafai, viburi, jeuri, kutosikiliza na kutotatua changamoto zinazowakabili wanachama kwa wakati muafaka.

Ndugu wanachama wenzangu, kwa hayo machache nashukuru moyo wenu wa upendo kwangu na kwa viongozi wenzangu wateule, kwa niaba yao tunaahidi kuchapakazi kwa maslahi yenu”amesema.

Katika uchaguzi  huo jumla ya kura 63 zimepigwa na zilizoharibika ni 8 ambapo Mwenyekiti wa Uchaguzi huo Abubakari Famau akizungumza na mtandao huu amewashukuru viongozi wapya waliochaguliwa huku akiwataka kufanya mapinduzi makubwa ndani ya chama hicho cha Waandishi wa Habari.

Naye ,Mwenyekiti    Mstaafu wa CPC Habel Chidawali kutoka Gazeti la Mwananchi ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wapya walioshinda.

“Kwa dhati ya Moyo wangu nawapongeza nyote mlioshinda  na kutangazwa  na mlioshinda lakini kura hazikutosha,mchuano hakukuwa cha mtoto  na hata waliobeza mfumo  wameona demokrasia  iliyotamalaki,ahsante Famau na timu yako  Mungu awabariki”amesema Chidawali.

Naye ,Daniel Mkate kutoka EATV   ambaye alikuwa mgombea nafasi ya uenyekiti lakini kura hazikutosha ametumia fursa hiyo kuwapongeza washindi pamoja na wapiga kura”ahsanteni kwa wale mliothubutu kunipigia kura na wale ambao hamkunipigia  Mungu awabariki wote tusonge mbele tuijenge CPC  Mawazo yetu yanatosha kukiweka chama Salama”amesema.

Katika uchaguzi huo ,nafasi ya uenyekiti jumla waliopiga kura ni 63,kura iliyoharibika ni 1,na wagombea  katika nafasi hiyo walikuwa ni watatu ambao ni Musa Yusuph aliyepata kura 23,Magnus Mahenge kura 20,na Daniel Mkate kura 19.

Nafasi ya Makamu mwenyekiti ilikuwa na mgombea mmoja tu kura zilizopigwa ni 63,kura iliyoharibika ni 1 ,kura za hapana 4  hivyo mshindi ni Mbashiru Katare aliyepata kura 58.

Nafasi  ya katibu mkuu ilikuwa na wagombea wawili ,ambao ni Bulaya Moses kura 25 na Benchine Bago kura 34 na kura zilizopigwa katika nafasi hii ni 63 na zilizoharibika ni 4.

Nafasi ya  Katibu Msaidizi ilikuwa na mgombea mmoja tu Mussa Enock ambapo amepata kura 59  kura za hapana 2 na zilizoharibika ni 2.

Na nafasi ya Wajumbe ilikuwa na  nafasi nne na waliojitokeza kugombea ni 3 ambapo Jasmine Shamwepu amepata kura za ndio 52,kura za hapana 10,na iliyoharibika 1,Doto Kwilasa amepata kura za ndio 47,kura za hapana 15 ,iliyoharibika 1 na Amani Mbando  amepata kura za ndio 51 ,kura za hapana 11na iliyoharibika 1.



Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: