Na Amon Mtega ,Songea

  BAADHI ya madereva wa magari ya abiria (Daladala) Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma bado wamekuwa wakikiuka maagizo yalitolewa na Serikali dhidi ya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

 Akizungumza  na  mhakiki wa usalama katika maeneo ya vituo vya mabasi ,Philopo Paswelo amesema kuwa ,bado kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya madereva hao kutokutii maagizo ya Serikali ya kuwataka kila dereva kwenye gari lake kuweka vitakasa mikono (Sanistaiza)kwaajili ya abiria.

  Paswelo ambaye pia naye ni dereva wa magari ya abiria ndani ya manispaa ya Songea amesema kuwa licha ya madereva hao kutokuweka vitakasa mikono kwenye magari hayo bado wamekuwa wakifanya makosa mengine ya kubeba abiria zaidi kwa kuwasimamisha bila kujali idadi ya viti vilivyopo.

   Amesema kuwa kufuatia hali hiyo uongozi umejipanga kushirikiana na askari wa usalama barabarani kuona namna ya kuwadhibiti madereva hao hasa katika nyakati za jioni ili kuwapa adhabu zilizowekwa kwa lengo la kuikomesha tabia hiyo.

    Paswelo amesema kua mapema mwezi huu mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipita na kamati yake ya ulinzi na usalama  pamoja na watalaamu wa afya  kutoa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona lakini baadhi ya watu wakiwepo madereva wa abiria wamekuwa wakishindwa kutii maelekezo hayo.

  Amefafanua kuwa baadhi ya madereva ambao wamekuwa hawazingatii maagizo hayo huku makondakta wao wakionyesha viburi na kuwajibu maneno ya jeuri kwa baadhi ya abiria ambao wamekuwa wakiwaelekeza namna ya kuzingatia maagizo ya serikali hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MWISHO.
Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: