Na WAMJW- MBEYA.

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuwaasa madereva wa vyombo vya usafiri kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati wa uhamasishaji kwa wananchi wa kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika Mikoa ya Mbeya na Songwe.

Amesema kuwa, kila dereva na kondakta wake ni lazima wahakikishe gari linakuwa na vitakasa mikono (Sanitizer) kwa ajili ya matumizi yao na abiria. Aidha, vituo vyote vya mabasi viwe na sehemu za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwa hii ni hatua muhimu sana ya kujikinga na virusi vya Corona. Aliyasema hayo alipotembelea Stendi Kuu ya mabasi katika Jiji la Mbeya iliyopo eneo la Nane Nane.

"Kondakta hakikisha kila anaepanda gari lako amenawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka au ametakasa mikono yake kwa Sanitizer ndio aruhusiwe kuingia kwenye gari, huu ugonjwa jamani ni hatari na umeua watu wengi" alisema.

Aidha, amewaagiza madereva na makondakta wao kuhakikisha kila siku jioni wanapokuwa wamemaliza kazi zao wahakikishe wanasafisha magari yao kwa dawa maalum aina ya Jiki, ili kuua virusi vinavyoweza kuwepo na kupelekea maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

"Madereva na makondakta wote kila siku jioni, hakikisha mnasafisha magari yenu kwa dawa maalum, wote mnaifahamu Jiki hapa, dawa hii inatumika Kutakasa magari, bajaji au pikipiki. Changanya kipimo kimoja cha Jiki na vipimo Sita (6) vya maji ili kupata mchanganyiko unaotakiwa kisha osha chombo chako cha kusafirisha abiria, utajikinga wewe na abiria wako " alisema.

Nae, Afisa kutoka Makao Makuu Jeshi la Polisi Kamisheni ya Ushirikishaji Jamii Stafu Sajenti Valentino Ngowi, amewataka madereva bodaboda kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watakutana na mtu alieingia nchini kwa njia za panya, ikiwa ni moja ya jitihada za kupambana na ugonjwa wa Corona, huku akiwataka wasiingie katika vishawishi vya kutaka pesa ya haraka ambayo inaweza kuwagharimu wao na taifa kwa jumla.

"Sasa hivi kuna abiria wengi ambao wanaingia mkoani Mbeya kwa kupita njia za panya, na njia rahisi wanayotumia ni watu wa Bodaboda, hivyo tunawata msiingie kwenye vishawishi vya kutafuta hela ya haraka kwa kuwapitisha watu hao, jambo ambalo ni kinyume na Sheria" alisema

Mbali na hayo, Stafu Sajenti Valentino Ngowi amewataka madereva wote wa vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata Sheria bila shurti, ikiwemo kuhakikisha abiria hawasimami kwenye magari (level seat), huku kwa upande wa Bajaj wapande abiria watatu tu.

Kampeni hii ya "Mikono safi, Tanzania salama" inaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana ya Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR. Katika kuchagiza ufikishaji wa elimu ya tahadhari dhidi ya Corona, Wizara inashirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery, ambae aliwakumbusha wakazi wa Jiji la Mbeya hususani maeneo ya Uyole, Sae, Ilomba, Mwanjelwa, Stendi Kuu, Meta, Nzovwe na Mbalizi kuzingatia unawaji wa mikono kwa maji na sabuni na vile vile kuepuka kushikana mikono na misongamano isiyokuwa na lazima. Ziara hii ya utoaji wa elimu ya tahadhari dhidi ya Corona inaendelea katika Mkoa wa Songwe ambao unapakana na nchi ya Zambia.

Mwisho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: