Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Kwa mwaka wa fedha 2019/20 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi
bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na katika kipindi cha
Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi
bilioni 527.31 ambayo ni asilimia 69 ya makisio ya mwaka.

Uchambuzi wa taarifa za mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi
cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 umeonesha ongezeko la mapato
yaliyokusanywa kutoka Shilingi Bilioni 449.82 kwa kipindi cha Julai, 2018
hadi Machi, 2019 na kufikia Shilingi bilioni 527.31 katika kipindi cha Julai,
2019 hadi Machi, 2020 ambalo ni ongezeko la Shilingi bilioni 77 sawa na
asilimia 17 .

Vile vile uchambuzi unaonesha kuwa katika kipindi cha Julai, 2019 hadi
Machi, 2020 Halmashauri 58 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia
75 au zaidi kwa kulinganishwa na makisio kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Aidha, Halmashauri 96 zimekusanya asilimia 50 au zaidi lakini chini ya
asilimia 75 na Halmashauri 31 zimekusanya chini ya asilimia 50 ya makisio
ya mwaka.

Halmashauri hukusanya mapato mengi au kidogo kwenye vyanzo tofauti
kulingana na hali halisi ya shughuli za kiuchumi za kila Halmashauri
ikiwemo mavuno na mauzo ya mazao mbalimbali na katika kipindi hiki
ushuru wa Huduma umekusanywa vizuri na umechangia asilimia 26 ya
mapato yote katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 na usimamizi
wa ukusanyaji wa mapato katika eneo hili unaonekana kuimarika.

Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya Halmashauri Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais – TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo mapema leo amesema katika
kipindi cha miezi tisa (Julai, 2019 – Machi, 2020), Halmashauri ya Mji wa
Njombe imevunja rekodi kwa kukusanya mapato kwa asilimia 130 ya
makisio ya mwaka 2019/2020 huku Halmashauri ya Wilaya ya

Shinyangaikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 30 tu ya makisio yake
kwa kipindi cha miezi tisa.

Mhe. Jafo alifafanua kuwa halmashauri zote zilizokusanya zaidi ya asilimia
100 hadi Machi, 2020 na zile ambazo zimejitathmini na kuona upo
uwezekano wa kuzidi asilimia 100 ya bajeti za mapato ya ndani ifikapo
Juni, 2020 zinaelekezwa kufanya mapitio ya Bajeti kwa mujibu wa Kifunga
cha 29 (1) cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ili ziweze kuongeza Bajeti
za mapato na matumizi ya fedha hizo.

“Halmashauri itakayoshindwa kufanya hivyo haitaweza kutumia fedha hizo
kwa kuwa Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 imekwisha idhinishwa na
Bunge” alisisitiza Jafo.

Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato
ghafi), Waziri Jafo ameeleza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya
Shilingi 43.14 na Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imekusanya mapato
kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 343.70.

Aidha Waziri Jafo amesema mapato ya ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa
kuzingatia asilimia kuwa Mkoa wa Njombe umefanya vizuri kwa kukusanya
wastani wa asilimia 87 ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo huku Mkoa
wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Simiyu ambao umekusanya
wastani wa asilimia 51 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo.

Katika kigezo cha mapato ya ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa kuzingatia
wingi wa Mapato amesema Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa
kukusanya kiasi cha Shilingi 126.77 huku Mkoa wa mwisho katika wingi
wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Rukwa ambao umekusanya
Shilingi 6.34.

Jafo alibainisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa
kuzingatia aina za Halmashauri kwa Kigezo cha Asilimia ya Makusanyo
ukilinganisha na makisio kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
imeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa
asilimia 78 ya makisio yake ya mwaka huku halmashauri ya Jiji la Dodoma
ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 55 ya makisio yake.

“Kwa upande wa Asilimia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeongoza
kundi la Halmashauri za Manispaa kwa kukusanya asilimia 100 ya makisio
yake huku Manispaa ya Lindi ikiwa ya mwisho akwa kukusanya asilimia 49
kwa mwaka wa Fedha 2019/20” amesema Jafo.

Katika kipengele cha Halmashauri za Miji, Jafo amesema Halmashauri ya
Mji wa Njombe imeongoza kwa kukusanya asilimia 130 ya makisio ya
mapato ya ndani kwa mwaka na Mji wa Handeni imekuwa ya mwisho kwa
kukusanya asilimia 43 ya makisio yake kwa mwaka.

Aidha, kwa kundi la Halmashauri za Wilaya amesema, Halmashauri ya
Wilaya ya Masasi imeongoza kwa kukusanya asilimia 126 ya makisio ya
mapato ya ndani na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imekuwa ya
mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 30 ya makisio ya mapato
yake ya ndani.

Waziri Jafo aliongeza kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya
Halmashauri kwa kuzingatia wingi wa makusanyo ni Jiji la Dodoma ambalo
limeongoza kundi la Majiji kwa kukusanya Shilingi bilioni 36.04 na
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam limekuwa la mwisho ambapo kwa
kukusanya Shilingi bilioni 8.83.

Kwa upande wa Manispaa, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeongoza
kwa kukusanya Shilingi bilioni 43.14 na Manispaa ya Kigoma Ujiji imekuwa
ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 1.20
amesisitiza Jafo.

Pia aliongeza kuwa halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa
mapato kwa kukusanya Shilingi Bilioni 7.02 na Halmashauri ya Mji wa
Mbulu imekuwa ya mwisho katika kundi kwa kukusanya Shilingi Milioni
671.78.

Na kwenye Halmashauri za Wilaya, Halmashauri ya Chalinze
imeongoza kwa kukusanya mapato mengi ya Shilingi Bilioni 5.78 na
Halmashauri ya Wilaya ya Gairo imekuwa ya mwisho katika kundi hili
ambapo imekusanya Shilingi Milioni 343.70.

Halkadhalika Jafo alibainisha matumizi ya vyanzo vya ndani vya
Halmashauri kwa kipindi cha Julai 2019 – Machi 2020 kuwa Halmashauri
zimetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 329.53 ambayo ni asilimia 63 ya
mapato halisi yaliyokusanywa na kati ya matumizi hayo, Shilingi Bilioni

186.75 zimetumika kwenye matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni
142.80 zimetumika kwenye matumizi ya maendeleo.

Amehitimisha kuwa Shilingi Bilioni 34.83 zimetumika kwenye miradi ya
maendeleo ikiwa ni bakaa ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha
2018/19 ambayo ni asilimia 76.5 ya bakaa yote (Shilingi Bilioni 45.54),
hivyo kufanya jumla ya matumizi ya miradi ya maendeleo kufikia Shilingi
Bilioni 169.20.
Share To:

Post A Comment: