Sunday, 8 March 2020

NAIBU WAZIRI MHANDISI NDITIYE ASEMA WACHINA TANZANIA NA CHINA NI RAFIKI HAWATAWAZUIA KUINGIA NCHINI ...


NAIBU waziri wa Uchukuzi na mawasiliano mhandisi Atashasta Nditiye amesema  Tanzania na China ni marafiki haitawazuia kuja nchini zaidi na wachina wanaokuja nchini kwa sasa hawakimbii virusi vya Corona kwao wanarejea kuja kuendelea na kazi walizoziacha .

Alisema kuwa umakini wa kuwapima umeongezwa katika maeneo ya viwanja na ndege ,bandari na mipanani ili kuona wageni wanaoingia nchini wanachunguzwa kama wana maambukizi ya virusi vya Corona ili wasiingize nchini  .

Mhandisi Nditiye aliyasema hayo leo  wakati akijibu maswali ya wanahabari mkoani Iringa baada ya kukamilisha uzinduzi wa mnara wa simu wa kampuni ya Haloteli katika kijiji cha Isoliwaya kata ya Ihimbo wilaya ya Kilolo .

Alisema kuwa wametengeneza miundo mbinu mizuri katika maeneo yote ambayo wageni wanaingia ili kuweza kuwaona na kuwapima kabla ya kuingia nchini .

"Tumeweka utaratibu kuanzia viwanja vya ndege ,bandari hata kwenye stesheni zetu na maeneo mengine kuona hakuna virusi vya Corona vinavyoingizwa nchini maana tunawapima na kuwaweka karantini kwa siku 14  mujibu wa taratibu zinazotakiwa za umoja wa kimataifa "

Alisema yapo makubaliano kuwa mtu anapotoka China lazima baada ya kupimwa awekwe chini ya uangalizi kwenye karantini maalum kwa siku 14 kabla ya kuruhusiwa na wamekuwa wakifanya hivyo .

Hata hivyo alisema kumekuwepo na ushirikiano mkubwa sana na wageni wanaotoka nchini China katika utekelezaji wa zoezi hilo na ndio sababu kubwa inayopelelea hadi sasa anamshukuru Mungu Tanzania kutokuwa na mgonjwa hata mmoja wa Corona.

Naibu waziri huyo alisema hadi sasa sekta ya uchukuzi na mawasiliano nchini haijayumba kwa Corona kutokana na ufanisi mkubwa uliowekwa na anaamini sekta hiyo haitayumba.

Aidha alisema kuwa suala la  wachina kuingia kuja nchini amewataka watanzania kutokuwa na hofu na sio kweli kama wachina hao wanakimbia Corona kwao kama watu wanavyosema ila wanarejea nchini kukamilisha miradi mbali mbali ya ujenzi wanayoijenga.

Alisema wachina wamekuwa na kawaida ya kila mwaka kurudi nchini kwao kula sikukuu na baada ya sikukuu kwisha wamekuwa wakirejea nchini na sio kweli kama wanaokuja nchini wanakimbia Corona kwao .

"Hebu niwaambie kitu kimoja wachina huwa wanakuwa na sherehe yao ambayo hufanyika mwezi February kila mwaka na sio Januari hivyo walikuwa umeondoka na sasa wanarejea nchini kuja kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo nchini kwetu "

Alisema kuwa serikali haiweze kuwazuia raia kutoka china na nchi nyingine duniani Kuja nchini kwani kila mgeni anayetaka kuja nchini anakaribishwa kuja Tanzania .

Katika hatua nyingine mhandisi Nditiye amewataka wale wote waliotumia namba zao za vitambulisho za Taifa (NIDA) kuwasajilia marafiki zao laini za simu kujisalimisha kwenye makampuni ya simu ili kufuta usajili huo kabla ya sheria kuchukua mkondo wake .

Pia aliwataka watumiaji wa simu wenye vitambulisho vya NIDA kuhakiki namba zao kama zinatumiwa na watu wengine ili kuzifunga namba hizo kabla ya namba hizo kufanya makosa yatakayopelekea mwenye kitambulisho cha NIDA kilichotumika kusajili kuwajibika.

Hata hivyo ametoa onyo kali kwa vijana wanaosajili laini za simu kwa alama za vidole kuacha kutumia kitambulisho cha NIDA cha mteja kusajili laini zaidi za kuuza .

Akielezea kuhusu mkakati wa wizara yake kukamilisha mawasiliano ya simu vijijini alisema wamejipanga kufikisha mawasiliano katika vijiji vyote Tanzania .

Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto akishukuru serikali kwa kufanikisha mawasiliano katika jimbo hilo alisema hadi sasa maeneo mengi wananchi wanapata mawasiliano ya simu na vijiji vichache kama Ilambo Kata ya Ibumu ndiko kuna shida ya mawasiliano.

Kwa upande wake mtendaji mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote(UCSAF Justina Mashimba alisema kwa mkoa wa Iringa jumla ya minara 33 imejengwa kwa kutumia ruzuku ya serikali

No comments:

Post a comment