Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Jeshi la Magereza nchini limedhamiria kuanzisha Kiwanda cha Mikate kitakachojengwa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga ili kwenda sambamba ya dhana ya Viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli.

Hayo yamesemwa leo Machi,20  na Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa Jeshi hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Ambayuu Kitiku wakati akiwasilisha maelezo ya Randama kuhusu Makadirio ya Mapato, Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo kwa mwaka 2020/2021 mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

“Katika mpango wa bajeti wa mwaka 2020/2021 Jeshi limeweka vipaumbele katika maeneo ya ajira na maendeleo ya watumishi, utawala wa magereza, uboreshaji miundombinu ya majengo ya magereza, kuimarisha shughuli za kilimo ili kujitosheleza kwa chakula, kuimarisha shughuli za Shirika la Magereza na kuimarisha shughuli za Viwanda ikiwepo Ujengaji wa Kiwanda cha Mikate kitakachojengwa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga kilichopo jijini Dar es Salaam” alisema SACP Kitiku

Akizungumza wakati akichangia hoja hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene aliwataka Jeshi la Magereza pindi mradi huo utakapoanza watengeneze mkate bora wakizingatia suala nzima la masoko, teknolojia bora ikiwepo ladha ya mkate huo, vifungashio vyake ili waweze kwenda sambamba na hitajio la mtumiaji wa mwisho

“Ni wazo zuri kwa mlichopanga kwani mtakapofanikiwa mtakua mmeongeza kipato na ile dhana ya jeshi la magereza kujitegemea itakua sasa imeingia kwenye utekelezaji sambamba na kujitosheleza kwa chakula cha kulisha wafungwa, lakini katika mpango huo lazima baadhi ya mambo muyafanyie utafiti ikiwepo soko linataka nini, teknolojia mtakayotumia muhakikishe ni nzuri itakayowafanya mpate bidhaa yenye ladha nzuri sambamba na kifungashio cha bidhaa hiyo, ni vizuri mmeliweka wazo wazi mapema nadhani mtapata michango ya kuliboresha” alisema Simbachawene

Jeshi la Magereza limeomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 201,251.298,000/- katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo huku likiweka lengo la kukusanya maduhuli ya Shilingi 2,000,000.000/- kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: