Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia), akibadilishana mkataba na Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel baada ya kusaini mkataba kwa ajili ya maandalizi ya kutoa huduma ya T- Hakiki ambayo ni maalumu kwa wakulima na wafugaji kuhakiki kwa njia ya simu viuatilifu vilivyosajiliwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia), na Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel wakionesha mikataba walioisaini kwa ajili ya maandalizi ya kutoa huduma ya T- Hakiki ambayo ni maalumu kwa wakulima na wafugaji kuhakiki kwa njia ya simu viuatilifu vilivyosajiliwa. 
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia), Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel (kushoto) na Mkurugenzi wa Biashara Quincewood, Fatma Fernandes (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusaini mikataba ya kwa ajili ya maandalizi ya kutoa huduma ya T- Hakiki ambayo ni maalumu kwa wakulima na wafugaji kuhakiki kwa njia ya simu viuatilifu vilivyosajiliwa. 
 

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI) zimeingia makubaliano ya maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa kuhakiki viuatilifu kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki. 

Mfumo huo uliopewa jina la ‘T–Hakiki’ ni huduma ya simu ya mkononi ambayo itamuwezesha mkulima kupata taarifa ya kiuatilifu kilichosajiliwa na kwa matumizi sahihi ili kuleta tija katika kilimo 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Kezia Katamboi alisema baada ya makubaliano hayo, utoaji wa huduma hiyo unatarajiwa kuanza mwezi ujao ikiwa ni baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu zinazotakiwa. 

Alisema makubaliano hayo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji na viwanda. 

Alisema hii ni hatua kubwa katika kulinda bidhaa za kilimo na ufugaji kwani itahakikisha wakulima na wafugaji wanapata mavuno yanayostahili. 

“Kwa kupitia mfumo huu ambao utatumia mawasiliano ya TTCL Corporation utakuwa suluhisho ya kuondoa viuatilifu feki sokoni na kuongeza kasi ya matumizi ya viuatilifu sahihi vya kilimo na ufugaji kwa kuwa mtandao wa TTCL Corporation umeenea nchi nzima hivyo wakulima wote nchi nzima watanufaika na mradi huu. 

“Zaidi ya yote huduma hii itapatikana bure kwa wakulima na wafugaji wote nchini. Kupata huduma hii, mkulima au mfugaji kupitia kwenye simu yake ya Mkononi, atabofya *148*52# kisha atafuata maelekezo,” alisema. 

Aidha, Mkurugenzi wa Biashara Quincewood ambayo inasimamia mfumo huo wa kuhakiki viuatilifu kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki, Fatma Fernandes alisema sekta ya kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi. 

“Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya Nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania. 

“Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi ya ndani, uuzaji nje ya Nchi na uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. 

Wakati Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropikia, Dk. Margaret Mollel alifafanua kuwa huduma hiyo ya “T-Hakiki” itamuwezesha mkulima kupata taarifa kuhusu viuatilifu vilivyosajiliwa na vyenye ubora unaotakiwa kwa kutumia hapo alipo kwenye sehemu yake ya kilimo. 

“Pia itamwezesha kujua matumizi sahihi ya viuatilifu kulingana na visumbufu lengwa kwa kuwasiliana na mamlaka ya TPRI pamoja na wamiliki wa viuatilifu na kutoa taarifa sahihi kwa TPRI kuhusu viuatilifu ambavyo havina ubora kwa ajili ya ufuatiliaji na kuchukua hatua,” alisema. 

Ubunifu wa huduma hiyo pia utaisaidia TPRI kutapa taarifa na ufuatiliaji wa urahisi wa viuatilifu wakati vikiwa sokoni pamoja na taarifa kutoka kwa mkulima yaani mtumiaji wa mwisho 

“Pia TPRI kama mdhibiti wa viuatilifu, T-Hakiki itafanya ufuatiliaji moja kwa moja bila hata kumshirikisha mtengenezaji au muingizaji wa kiuatilifu baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkulima moja kwa moja juu kiualitifu husika endapo kitakuwa hakifanyi kazi iliyokusudiwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: