Na GUSTAPHU HAULE, PWANI

KITUO cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kilichopo Kibaha Mjini kimeanza kujikita katika kufanya utafiti wa kufumbua mbegu  mpya za miwa zinazostahimili ukame.

Meneja wa kituo hicho Dr. Hildelitha Msita,aliwaambia waandishi wa habari juzi ofisini kwake kuhusu namna kituo cha TARI-Kibaha kinavyofanya shughuli zake.

Dr.Msita,alisema kuwa kituo cha TARI-Kibaha kimepewa jukumu la kuratibu na kusimamia tafiti zote zinazohusu zao la miwa na kwamba kwa muda mrefu hakufanyika tafiti za mbegu zinazostahimili ukame.

Alisema,mbegu  zilizopo hivi sasa ni zile ambazo zinafaa katika umwagiliaji ikiwemo N-19,N-25,N-30,N-41,R-570,R-575 na R-579 ambazo nazo zilifanyiwa utafiti kwa wakati tofauti tofauti kuanzia mwaka 2010 na 2014.

Dr.Msita,alisema kuwa mbegu za kustahimili ukame walianza kufanya utafiti rasmi mwaka 2013 na 2014  na katika utafiti huo wameona mbegu mbili zinafaa japokuwa bado hawajaeneza takwimu za kufanya zithibitishwe.

"TARI-Kibaha sasa hivi tumejikita katika kufanya utafiti wa kufumbua mbegu za miwa ya kutengenezea sukari ambazo zinastahimili ukame lakini tunakoelekea ni kuzuri kwakuwa tayari tumeona mbegu mbili zinauelekeo wa kufaa,"alisema Dr .Msita.

Aidha,Dr .Msita aliwashauri wadau wanaotaka kuanzisha viwanda vipya vya sukari kukikutumia kituo hicho ili wapate ushauri na teknolojia ya kuanzisha mashamba ya miwa kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

Hatahivyo,alisema kuwa mbali na kufanya shughuli za kiutafiti wa miwa lakini pia wanafanya tafiti za mazao ya mizizi ikiwemo Mihogo,Viazi na Viazi vikuu ambapo kazi hiyo inafanywa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo kikuu cha Dar es Salaam  na Chuo cha Kilimo cha Sokoine.

MWISHO
Share To:

msumbanews

Post A Comment: