Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, akikagua ukarabati wa madarasa katika Shule ya Msingi Mji Mkuu,(kulia) Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mji Mkuu Grace Malya.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, mhe. Abdulaziz Abood (kulia) akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mji Mkuu, Bi. Grace Malya (kushoto), Hundi ya Shilingi Milioni Moja na Laki Nne kwa ajili ya kuendeleza ukarabati wa madarasa matatu aliyoahidi ambapo awali alitoa shilingi Milioni 3 na laki 4 kutoka mfuko wa Jimbo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo akishuhudia makabidhiano hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo akisikiliza kwa makini taarifa ya ukarabati wa madarasa Shule ya Msingi Mji Mkuu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga (kulia) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, mhe. Abdulaziz Abood (kushoto) wakiteta jambo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa , RC Sanare ya ukaguzi wa madarasa yaliyofanyiwa ukarabati Shule ya Msingi Mji Mkuu.
Katibu tawala Wilaya ya Morogoro, Bi. Ruth John.
Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Michael Waluse, akielezea jambo wakati wa ukaguzi wa madarasa yaliyokarabatiwa Shule ya Msingi Mji Mkuu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mji Mkuu, Bi. Grace Malya, akisoma taarifa ya shule mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare.

Miongoni mwa majengo matatu yanayokarabatiwa kupitia mfuko wa fedha za Jimbo la Morogoro Mjini na fedha binafsi za Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Abdulaziz Abood.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare,  amewapongeza wadau kwa kufanikisha ukarabati wa madarasa chakavu katika shule ya Msingi Mji Mkuu iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya ,Morogoro.
Pongezi hizo amezitoa  wakati wa ukaguzi wa madarasa Manne chakavu yaliyokarabatiwa chini ya ufadhili ambapo madarasa mawili yametokana na ufadhili wa Mhe. Abdulaziz Abood Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia mfuko wa jimbo na mengine mawili chini ya ufadhili wa Nashela Hotel.
Katika ukarabati wa madarasa hayo , Mfuko wa Jimbo la Morogoro Mjini uliweza kuchangia shilingi Milioni 3 na laki 6 na fedha binafsi kutoka kwa Mhe. Abood ni shilingi Milioni 1 na Laki 4 huku ufadhili wa Nashela Hoteli ukitumia takribani shilingi Milioni 10.
"Napenda kutoa pongezi zangu za shukrani kwa wadau wote, haswa Mhe. Abood na Nashela Hotel, kwakweli shule hii ipo barabarani njiani kabisa nilipiga kelele lakini leo angalau ilifikia wakati nikamwambia Mkuu wa Wilaya tuifunge shule hii wanafunzi na walimu tuwahamishe lakini sasa inaonekana kufufuka , niombe Manispaa iangalieni shule hii kwa jicho la huruma ikiwezekana tafuteni pesa haraka kukoa jahazi hali sio nzuri viongozi wanapita njia hii ni aibu kubwa " Amesema Sanare.
Amesema mikakati yake ni kuhakikisha Watoto wote waliofaulu wanaenda shule na wanakaa kwenye madawati na atazunguka kila kata kuona hali ilivyo.
Pia ameendelea kusisitiza kwamba wale walimu Wakuu waliodumu muda mrefu bila ya matokeo mazuri ya ufaulu watashushwa vyeo na kuwa walimu wa kawaida.
Aidha , amesema Walimu ambao hawako shuleni bila taarifa za msingi wakatwe mishahara yao pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Pia amewaagiza Maafisa elimu wasaidiane na Wadhibiti ubora wa elimu ili kuleta matokeo chanya ya viwango vya ufaulu katika Mkoa wa Morogoro.
"Tunachotaka ni matokeo, yapo malalamiko mengi shuleni wananchi wanaonewa wakati Serikali ilishatoa maelekezo lakini hayatekelezwi, hivyo hatutakuwa tayari kuwaadhibu wadhibiti ubora wakati wapo waratibu wa elimu, niwaombe waratibu wa elimu wasimamie shule na sitotaka kusikia malalamiko kwani kikwazo cha kwanza katika kuchangia matokeo mabaya ya elimu ni watendaji "Ameongeza RC Sanare.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ameuagiza uongozi wa Kata ya Mji Mkuu kuhakikisha wanaitisha Vikao vya kuongea  na Wananchi wao kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya elimu na katika vikao hivyo wawashirikishe Mkuu wa Wilaya, Meya na Mkurugenzi ili watoe hamasa.
Amewataka waalimu na watendaji kuhakikisha kila mtu anafanya majukumu kwa nafasi yake huku akiwataka watendaji pamoja na maafisa elimu kuhakikisha kila kinachoingia na kutoka wakisimamie kwa misingi ya sheria na kanuni.
Katika ukarabati wa madarasa chakavu  , utengenezaji huo ulihusisha marekebisho ya sakafu, ukarabati wa kuta za ndani na nje (plasta), ubadilishaji wa silingi bodi (ceiling board), kenchi, uezekaji wa paa jipya, upigaji rangi wa madarasa mawili, wiring na umeme kwenye madarasa mawili pamoja na taa za kuongeza ulinzi mbele na nyuma ya madarasa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: