Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Katika kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wa shule za msingi ambayo ni mafanikio ya Elimu bure Serikali imeongeza uboreshaji wa miundombinu kwa kujenga shule za 243 kuanzia mwaka 2016.

Miongoni mwa shule hizo zipo shule Nnne za mfano ambazo zimejengwa katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kigoma na Mtwara.

Shule hizo za mfano zimejengwa maeneo yenye idadi kubwa ya watoto wanaoanza elimu ya awali sambamba na msingi na zina vyumba vya madarasa  vipatavyo 17, jengo la utawala, ukumbi wa mikutano, bwalo la chakula, jengo la kujisomea(library) pamoja na viwanja vya michezo.

 Kwa upande wa shule mpya ya mfano inayojengwa katika Mkoa wa Dodoma, Mweli amesema imejengwa ili kuondoa msongamano katika shule zilizodiwa na wanafunzi.

 Amesema shule hiyo itakayojulikana kwa jina la Mtemi Mazengo itakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 705, ikiwa wanafunzi 75 watakuwa wa elimu ya awali ambao watakuwa kwenye mikondo mitatu na wanafunzi 630 watakuwa ni wanafunzi wa darasa la Kwanza hadi la saba.

“ Hii ni moja ya shule ambazo zinajengwa kukabiliana na msongamano wa wanafunzi  ambao umetokana na uamuzi wa Serikali wa kutoa elimu bila malipo.”

Naye Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika jiji la Dodoma, Joseph Mabeyo alisema ili kuwapata wanafunzi watakao soma katika shule hiyo, umetumika utaratibu wa kukagua kadi za maendeleo na matokeo ya mitihani ya ndani ya shule(mihula) ya wanafunzi husika na kujiridhisha na uwezo wa kielimu wa wanafunzi husika.

 Alitaja shule ambazo wanafunzi wake wametoka na idadi ya wanafunzi kwenye mabano kuwa ni Shule ya msingi Ipagala (185), Ipagala B (355), Chadulu (70), Medeli (25, Mlimwa ‘C’ (70).

 Kwa upande wa walimu, Mabeyo alisema jumla ya walimu 20 watahitajika kufundisha katika shule hii na kwamba walimu hao watahamishwa kutoka shule mbalimbali za jiji kwa kuzingatia uwezo, nidhamu na uwajibikajiili kuleta ubora wa elimu.

Katika mwaka wa fedha 2018/2019, halmashauri ya Jiji la Dodoma lilipokea kiasi cha Sh milioni 706.4 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya mfano ya Mtemi Mazengo katika Kata ya Ipagala na ambayo imekamilika na itafunguliwa hivi karibuni.
Mwisho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: