Monday, 6 January 2020

TRIONI 6 KUJENGA KITUO CHA MICHEZO YA MAAJABU YA UTALII DUNIANI MJI WA LAMADI

Mfano wa moja  ya Disneyland  zilizopo kwa sasa ambazo zinaingiza watalii wengi mji wa kitalii Lamadi 
Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse

Mbunge wa jimbo la  Busega, Dkt. Rafael Chegeni

NA ANDREW CHALE, BUSEGA

Imeelezwa kuwa kiasi cha fedha   shilingi trilioni 6, zinatarajiwa kutumika mpaka kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha michezo cha maajabu ya Utalii (Disneylan) katika mji wa Lamadi, Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu.

Wakizungumza mjini Lamadi kwa nyakati tofauti wakati wa tamasha la kukuza na kuendeleza Utalii la Lamadi Utalii Festival, Mbunge wa jimbo la Busega, Dkt. Rafael Chegeni amesema ujenzi huo unatarajia kuanza mwaka huu na wataanzia na fedha za awali kiasi cha shilingi Trilioni  mbili (2) ambapo itaitwa 'Serengeti Disney'

"Fedha za awali trilioni mbili tutaanzia mradi huu. Lakini mpaka kukamilika kwake utagharimu jumla ya trilioni 6.  Serikali ya John Pombe Magufuli inafanya kazi na mradi huu utakuwa chachu ya kiuchumi katika nchi" alisema Dkt. Chegeni.

Naye Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania alisema kuwa, Mji huo wa Lamadi utakuwa unapokea watalii zaidi ya 5,000 kwa mwaka huku ukiwa mji pekee Bara la Afrika utakaokuwa ukiingiza fedha nyingi za kigeni utakapokamilika ujenzi wa Disneyland.

"Mradi huu kwa duniani utakuwa wa Saba. Kwa hiyo mji wa Lamadi utakuwa ukipokea fedha nyingi za kigeni kwani Watalii zaidi ya 5,000 watakuwa wakitembelea kila mwaka.

Nchini Marekani kwenye Disneyland yao kule miji ya Florida na California  wanapokea watalii zaidi ya 10,000 kwa mwaka. Nilikuwa huko miezi ya Sita na Saba. Sasa wageni wa mataifa ambapo hakuna Disneyland  watakuwa wanakuja hapa Tanzania  Busega Simiyu katika mji wa  Lamadi.

Mabenki, hoteli na uwekezaji katika utalii fursa zianze sasa katika mji wa Lamadi" alieleza Dkt. Kibesse.

Kwa upande wake, Meneja wa Pori la Akiba la Kijereshi ambapo mradi huo utajengwa,  Diana Chambi ametoa wito kwa jamii kulinda uhifadhi ili uweendelevu kwa vizazi vyote vya sasa na vijavyo ambapo pia ametoa wito kwa wadau wa utalii kutembelea kwa lengo la kuimalisha  Utalii wa ndani.

Miongoni mwa Disneyland sita ambazo zipo hadi sasa ni pamoja na :

Nchi ya Marekani ina Disneyland mbili katika
Disneyland Park, Anaheim California na Walt Disney Orlando Florida.

Disneyland Paris, (Ufaransa), Hong Kong Disneyland,  Tokyo Disneyland, (Japani) na  Shanghai Disney (China) hivyo inayotarajiwa kujengwa Lamadi itakuwa ya Saba na itakuwa ya kisasa kutokana na eneo lake kuwa katika hifadhi yenye wanyama na Ziwa (Ziwa Victoria).

No comments:

Post a comment