Sunday, 26 January 2020

DC WA CHUNYA AMALIZA MGOGOLO ENEO TENGEFU LA MATAFLA

 mkuu wa wilaya hiyo akifafanua jambo kwa wananchi kuhusiana na mgogoro huo jinsi ulivyotatuliwa
wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Chunya Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa mkutano wa hadhara wa utatuzi wa mgogoro huo
...................................................
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhandisi Maryprisca Mahundi amefanikiwa kutatua  mgogoro baina wananchi ,serikali ya kijiji na wawekezaji wawili Singu Duwila na Staphord Mwanzyala katika eneo tengefu la Matafla mwandishi  Esther Macha anaripoti kutoka Chunya

Wawekezaji hao waliopatiwa leseni ya uchimbaji madini na Wizara ya Madini kwa ajili ya kuchimba wamekuwa na mgogoro tangu kufanikiwa kukilipa kijiji cha Sangambi shilingi milioni kumi na tatu kati ya kumi na tano walizopatana katika eneo tengefu lililotengwa kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi hivyo kushindwa kufikia malengo yao kutokana na baadhi ya wananchi kudai kiasi kilichotolewa ni kidogo na baadhi wakidai eneo hilo lirejeshwe kwa kijiji ili kijiji ndicho kihusike na uchimbaji wa madini katika eneo hilo.

Akitoa ufafanuzi Afisa Madini Mkazi Wilaya ya Chunya Godson Kamihanda alisema leseni iliyotolewa kwa wawekezaji hao ni halali kwa mujibu wa sheria ya madini hivyo kama kuna mgogoro baina  yao ni vema wakaketi ili kuyamaliza malalamiko hayo ya pande zote.

Akichangia maoni yake Diwani wa Kata ya Sangambi Junjulu Mhewa huku akionesha ramani ya eneo tengefu ya Matafla alisema yeye hafungamani na upande wowote kutokana na mgogoro uliopo  hivyo ni vema wawekezaji hao wakaliachia eneo hilo ili kijiji kichukue leseni Wizara ya madini ili kijiji kiwapangishe watu watakaohitaji kuchimba eneo hili ili fedha zitskazopatikana zisaidie maendeleo ya kijiji na Kata kama ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari.

Junjulu alisema awali eneo hilo liikuwa na leseni kubwa lakini muda ulipokwisha wa mkataba wa wawekezaji walipaswa kulirejesha kijijini wawekezaji waliwazunguka na kwenda ofisi ya madini na kuchukua leseni na kijiji kutonufaika chochote hivyo alishauri wote wanaochimba eneo hilo wayarejeshe maeneo yote ili wote wanaohitaji kuchimba waombe upya.

Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Bosco Mwanginde alisema ni vema sheria zote zikafuatwa ili kuepusha migogoro isiyo na tija.

Mwanginde alisema ni vema pande zote zikakubaliana kuondoa tofauti zao kwa maslahi mapana ya Kijiji,Kata na Halmashauri kwa ujumla na kuwataka wananchi wawapate wawekezaji watakaojenga badala ya kutoa pesa taslim ambazo huleta marumbano katika kijiji.

Ambakisye Mwaisumo ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo alisema wawekezaji waliomiliki eneo hilo waendelee kwani pesa walizotoa zilichangia maendeleo ya kijiji yakiwemo madarasa hivyo kuwaondoa ni kitendo cha wivu.

Wakichangia maoni yao katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Majengo Mariam Ntangu na Adam Mwakalobo walisema wawekezaji hao wafikiriwe na wameshangazwa na kuwepo kwa mgogoro bali walisema kuna watu wanatengeneza mgogoro.

Mwakalobo alisema kwa kuwa mkataba wa wawekezaje umekwisha ni vema wakaongeza muda na wakaongeza pesa ili kijiji kinufaike.

Frank Mbwilo ni Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Kata ya Sangambi alisema yeye kama Mwenyekiti alipata kusuruhisha mgogoro huo ambapo aliwasihi wananchi kutatua kwa makini kwani imeonekana kuna baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji wanalihitaji eneo hilo kwa maslahi binafsi ambapo matokeo yake yanawaumiza wawekezaji ambao walihangaika mno kupata hiyo pesa ya kulipa kijiji.

 Aidha alishauri wawekezaji kulipa pesa zilizosalia kisha waombe upya kijiji ili wakikubaliana waendelee kuchimba kabla ya leseni zao kumalizika.

Pia ni vema wakafikiriwa zaidi wawekezaji hao kwa kuwa ni wazawa na pesa waliyoitoa wameiona na hilo halina ubishi alisema Mbwilo.

Akihutubia wananchi katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya Mhandisi Maryprisca Mahundi aliwaonya wananchi kuacha kutoa maamuzi kwa mihemko kwani inazorotesha maendeleo katika jamii.

Awali aliwasihi kuwafikiria wawekezaji hao wazawa ambao walifanikiwa kuchangia milioni kumi na tatu kati ya kumi na tano walizopatana hivyo wanapaswa kuwadai wawekezaji shilingi milioni mbili zilizosalia kabla ya kuanza mkataba mwingine.

Hata hivyo Mahundi aliwaomba wananchi kuwafikiria muda zaidi wawekezaji hao kwani muda mwingi waliutumia kujadili mgogoro huo na kushindwa kuchimba  madini katika eneo hilo tengefu la Matafla.

Alisema ni vema wananchi na serikali wakaorodhesha watu wote wenye leseni za uchimbaji katika msitu huo wa hifadhi ili kila mchimbaji achangie maendeleo yakiwemo ya ujenzi wa sekondari ya Sangambi.

"Msitu tengefu wa Matafla una zaidi ya wachimbaji mia mbili wenye leseni hivyo kama wachimbaji watachangia pesa za ujenzi wa shule ya Sangambi shule hiyo itakuwa ya mfano wa kuigwa katika Wilaya ya Chunya kwa kujengwa ubora"alisema Mahundi.


No comments:

Post a comment