Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, akizungumza na wafanyakazi wa Migodi ya Sekenke, (hawapo pichani) muda mfupi kabla ya kuufunga mgodi wa sekenke namba moja, uliopo halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida hivi karibuni. 
 Vitendea kazi vikiwa katika mgodi huo wa Sekenke namba moja.
 Mkuu wa Mkoa akikagua eneo la mgodi lililozama katika mgodi wa Sekenke namba moja halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Na Mwandishi Wetu, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi amefunga kwa muda mgodi wa ‘sekenke namba moja’  uliopo wilaya ya Iramba mkoani hapa kama tahadhari kupisha uchunguzi wa kina na kitaalamu kubaini chanzo kilichosababisha kutitia ghafla kwa sehemu kubwa ya udongo eneo hilo na kusababisha taharuki kwa wananchi
Akizungumza kupitia mkutano wa hadhara kwenye eneo hilo la tukio hivi karibuni, Dkt. Nchimbi alisema tangu kutokea kwa tukio hilo lisilo la kawaida juzi, kila alipojaribu kuhoji nini hasa kimesababisha eneo hilo kuzama, na kilichozama hapo ni udongo pekee au kuna watu wamefukiwa? Lakini mpaka sasa anapokea maelezo ya kugongana-gongana
 Alisema baadhi ya wamiliki wa maeneo hayo walimweleza kuwa kuzama (kutitia) huko kwa udongo kumesababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Wakifafanua kwamba maji ya mvua yalitiririka na kukutana na nyufa, na hatimaye kulainisha udongo uliokuwa umeshikana na nguzo, na kupelekea udongo kuachia na kutitia
“Nikiwa mkuu wa mkoa huu, tena mama ambaye ni lazima nisimame katika kuhakikisha usalama na mazingira mazuri ya kunufaika na haya ambayo Mwenyezi Mungu ametupa, kuanzia leo ninapafunga hapa, ninafunga mgodi namba moja kupisha uchunguzi wa kina mpaka pale mtakapopewa taarifa,” alisema Nchimbi na kuongeza;
“Ninafunga namba moja ila namba mbili iendelee. Nafunga sekenke namba moja hadi pale wataalamu wa madini watakapokuja kufanya uchunguzi kubaini kama chanzo cha kutitia huko ni mvua kweli, na kama kuna madhara mengine ikiwemo vifo,”
Aidha, Nchimbi akitoa tathmini yake binafsi juu ya alichokibaini kwenye eneo la tukio, alisema kilichosababisha kutitia kwa udongo huo ni ubinafsi, ni tamaa, uroho wa kutaka kupata fedha kwa haraka, na watu kukosa hofu ya Mungu, huku akisisitiza kuwa watu wa aina hiyo ndio waliolipua zile nguzo zinazoshikilia pale kwa makusudi
“Kuna nguzo pale tangu enzi za utawala wa Mjerumani zinazoshikilia, Mkoloni huyu pamoja na nguvu zake, pamoja na uwezo wake, na kwa kutambua eneo hilo la nguzo kuna dhahabu alisema endapo nitalipua hizi nguzo basi huu mgodi hautakuwepo, na hakuwahi kufanya hivyo,” alisema Nchimbi
Alisema anasubiri majibu ya wataalamu, ila sababu ya kwamba mvua imesababisha haimridhishi, kutokana na huko nyuma kuwapo na mvua nyingi zikiwemo za El-Nino lakini tukio kama hilo halikuwahi kutokea, huku akihoji kama ni mvua mbona sekenke namba 2 haijadhurika, mpaka sasa pako salama.
Aliwataka wafanyakazi hao kuwa na subira kupisha uchunguzi ili kubaini kwa haraka kama ni mvua kweli, na kama sababu itakuwa ni mvua basi atalazimika pia kuufunga mgodi huo kusubiri mpaka pale msimu wa mvua utakapomalizika. Aidha alisema kama ikibainika atakuwa amesababisha mtu basi atatamani ikiwezekana afutiwe kabisa leseni ya kujishughulisha na madini
Alisema mara kadhaa zinapotokea dhoruba kama hizo wanaokufa huwa ni wafanyakazi, huku wamiliki wa migodi na miduara hiyo wakiendelea kuwa salama. Alisema alipokuwa akiongea na wamiliki hao aliwauliza kwanini msiwe mnatangulia kufa ninyi? Maana wanafanya upuuzi sababu wao hawaingii huko
“Nataka niwahakikishie wafanyakazi Rais Magufuli anawapenda sana, na eneo hili lote mlimchagua kwa kura nyingi, fursa hii ya madini haikutolewa na serikali au kuruhusiwa ili watu wafe hapana! Tunataka madini yetu yasigeuke chanzo cha huzuni na maafa, bali yatuletee amani, furaha, maisha marefu kwa vizazi na vizazi…na hii ndiyo furaha ya taifa lolote lile ambalo linajipenda,” alisema Dkt. Nchimbi
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba ambaye eneo hilo ni sehemu ya jimbo lake, aliomba wananchi watoe ushirikiano wakati wote zoezi la ukaguzi litakapokuwa likiendelea, na kuwataka kuchukua tahadhari kuepuka athari nyingine inayoweza kujitokeza hata wakati wa uokoaji
“Pia ninaomba tupewe ruhusa kwa wale wenye mitambo yao hapo nje na wana mawe ambayo tayari wamekwisha yachimba basi waendelee kusafisha wakati taratibu nyingine zikiendelea…tupewe ruhusa ya kusafisha na sio kuchimba,” alisema Nchemba.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: