Saturday, 2 November 2019

WANANCHI WA MAGUNGUMKA WALA KIAPO KUWACHAGUA WAGOMBEA WA CCM SINGIDA

 Wananchi wa Kitongoji cha Magungumka Kata ya Mgungila wilayani Ikungi Mkoani Singida wakila kiapo jana katika mkutano wa hadhara mbele ya Mbunge wao Elibariki Kingu cha kuwachagua viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 24 mwezi huu.
Mbunge Kingu akihutubia kwenye mkutano huo.
 Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
 Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Wilaya ya Ikungi, Sanka Pius akizungumza.
 Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
 Viongozi wakiwa meza kuu kwenye mkutano huo.
 DC wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akizungumza.
 Watoto wakiwa kwenye mkutano huo.
 DC Mpogolo akifurahi na Diwani wa eneo hilo, Hussein Ng'enyi.
 Wanafunzi wakiwa kwenye mkutano.
Mkutano ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WANANCHI wa Kitongoji cha Magungumka Kata ya Mgungila Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wamekula kiapo mbele ya mbunge wao Elibariki Kingu na kusema watahakikisha kura zote za wagombea nafasi ya uenyekiti wa vijiji,  vitongoji na mitaa katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 24 mwezi huu kuwa zitakwenda kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Wameyasema hayo  jana katika mkutano wa hadhara aliouandaa mbunge wa jimbo hilo,  Elibariki Kingu wakati akikagua miradi ya maendeleo pamoja na kuwahamasisha kujiandikisha kwa wingi ili waweze kuwachagua viongozi  kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wananchi hao walisema hawaoni sababu itakayowafanya wasiwachague viongozi hao kutoka CCM.
" Hiki kitongoji chetu cha Magungumka hakikuwa na maendeleo kabisa hatukuwa na huduma muhimu kama zahanati, barabara, shule na maji lakini serikali yetu kupitia huyu mbunge wetu Kingu tumepata vitu hivyo sasa kwanini tusiwachague viongozi kutoka CCM" alisema mkazi wa kijiji hicho  aliyejitambulisha kwa jina moja la Shija.
Shija alisema walikuwa na changamoto kubwa ya barabara kwani wakati wa mvua za masika walikuwa wakitembea kwenye maji kutafuta usafiri wa  kwenda Singida mjini lakini hivi sasa kero hiyo haipo tena baada ya Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli kupitia Mbunge Kingu kuwajengea barabara.
Kingu akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na Katibu wa Uenezi na Itikadi  wa CCM wa wilaya hiyo, Sanka Pius alisema Serikali imetenga sh.300 milioni kwa ajili ya kusambaza maji katika kijiji hicho pia imetoa sh.47 milioni kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati ya kitongoji hicho.
Alisema tangu Rais Dkt. John Magufuli aingie madarakani katika kipindi cha miaka minne tu amefanya mambo makubwa  ameweza kusambaza miradi ya maji 24 katika jimbo hilo, kujenga barabara, zahanati, vituo vya afya na shule na maeneo mengine yamekwisha pata umeme.
" Ndugu wananchi heshima pekee ya kumpa Rais wetu kwa kutuletea miradi hii ni kuhakikisha tunakipa ushindi mkubwa chama chetu naombeni twendeni tukajiandikishe kwa wingi na siku ikifika ya kupiga kura basi tuwachague viongozi watakaounda serikali kupitia CCM" alisema Kingu.
Kingu katika mkutano huo alitoa mabati 117 na saruji mifuko 110 kwa ajili ya ujenzi wa nadarasa ya shule ya kitongoji hicho chenye wananchi wengi pamoja na choo.
DC Mpogolo akizungumza katika mkutano huo alisema amesikia ombi la kuongeza mda wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura kutokana na watu wengi kushindwa kujiandikisha kwa sababu  ya wingi wao na mashine kukorofisha na kueleza suala hilo atalipeleka kwa wahusika ili lifanyiwe kazi.
Katika hatua nyingine Mpogolo amewahakikishia usalama wananchi hao wakati wa upigaji wa kura katika uchaguzi wa viongozi wa vijiji na vitongoji utakaofanyika tarehe 24 mwezi huu na kuwa serikali imejipanga na mtu yeyote atakayejaribu kuleta vurugu atakiona cha moto.

No comments:

Post a comment