Wednesday, 6 November 2019

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KIGAMBONI SARAKASI TUPU, WAGOMBEA WA CHADEMA 67 WAENGULIWA MAJINA YAO BILA SABABU


Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya wagombea wa uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam wamepeleka kilio chao kwa wasimamizi kufuatia kukata majina yao  katika mitaa 67  na kupitisha wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  pekee kinyume na taratibu.

Mmoja wa waliokuwa wanagombea nafasi hiyo kupitia Serikali ya Mtaa wa Mbwamaji uliopo Gezaulole, Yohana Luhemeja ameonesha masikitiko yake baada ya kukatwa kwa majina hayo likiwemo jina lake bila sababu za msingi kitendo alichokiita kuminywa kwa Demokrasia nchini.

Mgombea huyo awali ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa huo, alieleza kuwa hajui sababu za jina lake kukatwa na wala kupewa sababu za msingi hivyo kulalamikia kamati zilizopewa jukumu hilo la kupitisha majina ya wagombea.

Akinukuliwa kufuatia hali hiyo:

"Kigamboni tuna Mitaa 67, yote tuliweka wagombea na majina yaliyorudi ni mawili tu na mengine 65 yamekatwa hii inaichafua Serikali kwani toka Demokrasia ya vyama vingi ianze Tanzania, kitu kilicho fanywa na  wasimamizi wa uchaguzi huu wa 2019 hakikufuata kanuni na sheria.

Kamati za siasa za Wilaya Watendaji mtaa zimeshiriki kutengua wagombea wa vyama vya upinzani na kuwateuwa wagombea wa CCM pekee.  Pia kuna sababu nyingi ambazo hazina msingi dhidi yetu kwa namna walivyotukata majina, Tanzania tunaipeleka wapi? kama vyama vingi havitakiwi Tanzania basi vifutwe vyote " alisema Yohana Luhemeja.

Aidha, alibainisha kuwa, tayari ameshakata rufaa na huku ikitarajiwa kukabidhi ndani ya muda wa taratibu za rufaa.

"Tayari viongozi wetu wa juu wameliona hili na tararibu zingine zinafuata ikiwemo kukata rufaa ambayo ni ndani ya muda wa siku tatu" alieleza.

Yohana  Luhumeja amemalizia kuwa, uchaguzi huu wasipoangalia watasababisha wananchi kuchaguliwa watu wasiofaa na mwisho kurudisha maendeleo nyuma ya mitaa.

Mwisho

No comments:

Post a comment