Sunday, 10 November 2019

Diwani Wa CHADEMA Ashirikiana na Viongozi Wa CCM Kukarabati BarabaraNa Ferdinand Shayo,Arusha.

Diwani wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CHADEMA kata  ya Maruvango  Digna John Nassari ameamua kushirikiana na wananchi ,wadau wa maendeleo pamoja na Viongozi wa CCM katika kukarabati na kufungua barabara za vijiji vilivyopo katika kata hiyo ambazo zilikua hazipitiki kwa kipindi kirefu na kusababisha adha kubwa hasa kwa wananchi hususan wagonjwa na wakinamama wajawazito kushindwa kufika katika huduma za afya kwa  wakati na hata kupoteza maisha.

Akizungumzia ukarabati huo Diwani huyo amesema kuwa  baada ya kuona adha wanayoipata kinamama kwenda sokoni na kufikia vituo vya afya wameamua kufungua barabara hizo ambazo baadhi zilikua katika hali mbaya ya kutokupitika kabisa lakini kwa sasa wameweza kuzifungua barabara hizo upya na wananchi wanapita bla shida.

Digna  amesema kuwa ameshirikiana na wananchi pamoja na wadau ambao wamechangia mafuta ya katapila,greda la kushindilia ambalo ni mali ya Halmashauri ya Meru  pamoja na fedha za kuwalipa madereva huku msaada mkubwa ukitoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Meru Jerry Muro pamoja na Wenyeviti wa vijiji ambao wengi wao ni wa CCM lakini kwa hili  wameshirikiana vyema kufanikisha ukarabati wa barabara.

“Niliwaita rafiki zangu nikawaomba wanichangie fedha kwa ajili ya mafuta kwa ajili ya magreda ambayo ,kampuni ya Arusha Agrigates walinipa mafuta lita 50,kampuni ya Lake Oil iliyopo maji ya Chai walinipa lita 100,King`ori Agrigates lita 100,Munio walinipa lita 50 kwa kweli nawashukuru sana wadau wa maendeleo kwa kunisaidia pia  Dc Muro alinisaidia kupata barua ya kuomba mchango wa wadau pia viongozi wa Vijiji wamenipa mafuta kwa ajili ya katapila”

Afisa Mtendaji wa Kata ya Maruvango Hassan Shomari Kupe amesema kuwa miaka ya nyuma barabara zilikua nyembamba hazipitiki zilikarabatiwa mwaka 1950  hata kinamama wajawazito walipata tabu kwenda kwenye zahanati ,lakini kwa sasa Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano Raisi Magufuli,Mkuu wa Wilaya na Diwani kwa kushirikiana nasi katika kufanikisha adhma hii ya kuwatumikia wananchi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbaseny Zablon Lucas amepongeza juhudi zilizofanywa na Diwani huyo ambazo zimewezesha barabara kupitika kwa urahisi hasa kwa wakulima kusafirisha mazao yao kuyapeleka masokoni.

Elly Elirehema Urio amesema kuwa barabara hiyo itakua mkombozi kwa kinamama kwani miaka mingi waliteseka na hawakupata barabara ila kwa sasa wana uhakika wa kuwa na barabara zitakazopitika kwa kipindi chote cha mvua na jua.

No comments:

Post a Comment