Watafiti nchini wameshauriwa kuwasilisha andiko lolote la utafiti kwanza kwa wadau wa utafiti kabla ya kuomba kibali Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH ili wadau hao waweze kutoa ushauri wao kuhusu utafiti unaofanywa kwenye sekta yao na hivyo kufanya tafiti kuwa na tija zaidi kwa taifa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa wakuu wa Taasisi za Elimu ya Juu na taasisi za Utafiti na maendeleo nchini kujadili kuhusu maadili, Taratibu,Sheria na kanuni za kufanya utafiti nchini iliyoandaliwa na COSTECH kwenyew ukumbi wa Taasisi ya elimu ya kujiendeleza kwenye Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.

Amesema ili tafiti ziweze kuleta tija zaidi na kuondoa changamoto za kurudia kufanya utafiti kuna kila sababu ya Watafiti kuwasilisha kwanza mawazo yao kwenye wizara au sekta husika kabla ya kupeleka maombi ya kufanya utafiti wowote kwenye Tume hiyo kwaajili ya kupitiwa na kupata kibali.

Dkt. Nungu amesema kumekuwa na lawama nyingi kwa baadhi ya watafiti kwamba vibali vya kufanya utafiti vinacheleweshwa na COSTECH kitu ambacho amesema inatokana na wao kuwasiliana na taasisi husika ama wadau wa utafiti kabla ya kupeleka kwenye kamati maalumu ya kitaifa kupitia na kuwapa ruksa ya kutoa kibali husika cha utafiti.

’’Mathalani unafanya utafiti kwenye Elimu tunategemea Utafiti wako utakuja kubadilisha ua kuboresha sera hivyo ni muhimu Wizara ya Elimu iweze kujua kinachofanyika ili nao waweze kutoa neno maana inawezekana ukafanya utafiti ambao majibu yao wanayo tayari’’ Alisema Dkt. Nungu.

Mkurugenzi huyo Mkuu wa COSTECH ameongeza kuwa eneo lingine ambalo  wadau hao watajadiliana na kutoa mapendekezo ya pamoja ni namna ambavyo Mtafiti wa ndani anavyotakiwa kushiriki kwenye utafiti wa watu kutoka nje ya nchi hasa baada ya kugundua kuwa watafiti wa ndani huandikwa tu kwenye makaratasi kukithi vigezo vya kufanya utafiti lakini hawashiriki na hawafahamu lolote kuhusiana na hatua na utafiti unavyofanyika.

‘’ Taratibu za mtu kufanya utafiti kutoka nje ya nchi zinamtaka mtafiti huyo kuwa na mtafiti kutoka Tanzania lakini cha ajabu mtafiti wa ndani unapomuuliza kuhusu utafiti unavyoendelea na hatua zilizofikiwa hana majibu anakuambia anajua mtafiti wa nje kitu ambacho sio sawa katika taratibu za vibali vya kufanya tafiti za aina hizo’’ Alifafanua Dkt. Nungu.

Dkt. Nungu amesema haya na mambo mengine mengi ndiyo yaliyotufanya tukusanyike hapa kama wadau ili tuweze kufahamishana na kupeana ushauri wa namna ya kuboresha namna ya utendaj kazi kwenye eneo la utafiti ili ziweze kuleta tija nchini.

Kwa upande wake makamu wa mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. Lugano Kusiluka ambaye ni mshirki wa warsha hiyo amesema utafiti unasaidia kutatua changamoto za nchi lakini pia lazima uzingatie vigezo na maadili ya kufanya taifi ili ulete tija kwa taifa.

Amesema ili Utafiti uingie na kutambuliwa na Taifa lazima upitie COSTECH ambao ndio waratibu wa tafiti zote ili kuweza kufikia malengo na serikali iweze kuutumia kwa manufaa ya jamii na Taifa badala ya watafiti kuishia kwenye taasisi zao kabla ya kushirikisha wadau.

Amesema kukutana kwao kwenye warsha hiyo kutasaidia sana wakuu wa taasisi kuweza kuwasaidia watafiti wake kutimiza vigenzo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za tafiti ili kuwa na Utafiti bora lakini pia kuwahisha kupata kibali kutoka COSTECH.
 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH Dkt. Amos Nungu akizungumza na Waandishi wa habaru nje ya ukumbi.
 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH Dkt. Amos Nungu akifungua Warsha hiyo.
 Makamu wa mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. Lugano Kusiluka akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mkutano.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH Dkt. Amos Nungu akizungumza na Waandishi wa habari nje ya Mkutano.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: