Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekipongeza Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuendesha Kongamano la kumkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kusema kuwa hili ni jambo jema sana.

Dkt. Kikwete amesema Mwalimu Nyerere anastahili sana kukumbukwa na wala siyo jambo la hisani maana amefanya mema mengi kwa  Watanzania, Waafrika na Ulimwengu kwa ujumla.

“ Mwalimu ndiyo mkombozi wetu, tulikuwa tunatawaliwa na wakoloni lakini aliamua kuacha kazi yenye mshahara na kuingia kwenye kupigania Uhuru kwa maslahi ya wengi,”anasema Mhe. Kikwete.

Dkt. Kikwete Amesema Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambacho miaka ya nyuma kilijulikana kama kivukoni  ndiyo chimbuko la mafunzo ya uongozi, maadili na uzalendo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Stephen Wasira amesema  utaratibu wa Chuo kufanya makongamano ya kuwaenzi waasisi wa Taifa pamoja na makongamano ya kitaaluma ni mambo ya Msingi sana kwa Taifa.

Wasira amesema shabaha ya makongamano ni kukumbuka ushujaa, uongozi na uzalendo waliokuwa nao waasisi wa Taifa, pia kupitia makongamano hayo  wanafunzi wanapata fursa ya kujua historia ya nchi na waasisi wake.

Alisema juhudi  za baba wa Taifa  kujenga nchi yenye umoja haikuwa ni bahati mbaya Bali ni dhamira ya kujenga umoja, Upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Naye Mkuu wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema
dira ya Chuo ni utoaji wa maarifa bora, ubunifu na kufanya tafiti kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali katika Jamii.

Prof Mwakalila amesema Chuo Cha Mwalimu Nyerere Kinatambua mchango wa Baba Taifa na ndiyo maana Chuo kimekuwa mstari wa mbele katika kuyaenzi yale aliyofanya Baba wa Taifa.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Habari na Mawasiliano,
Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
8/10/2019
Share To:

msumbanews

Post A Comment: